04 September 2014

WABUNGE 25 WA CCM WALIOJIUNGA UKAWA KUFUKUZWA UANACHAMA



Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. 

Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakusudia kuwachukulia hatua wabunge wake zaidi ya 25 kwa makosa ya kutoshiriki kikamilifu vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea Dodoma.

Mpango huo ulitangazwa juzi usiku na Katibu wa Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kwenye kikao kilichoitishwa kwa ajili ya kuwajulisha wabunge wa chama hicho mwongozo wa mjadala katika Bunge Maalumu.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Mhagama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alitoa maelezo hayo mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hata hivyo, mtoa habari wetu alisema Kinana hakuzungumza chochote zaidi ya kusikiliza hoja za wajumbe wa kikao hicho, wakati Pinda alitoa maneno machache ya ufunguzi na baadaye kufunga.

Alisema wabunge hao wataandikiwa barua wajieleze kwa nini hawafiki kwenye vikao vya Bunge Maalumu tangu limeanza.

Habari hizo zimepasha kuwa baada ya Mhagama kuanzisha hoja hiyo aliinuka Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ambaye alisema lazima suala hilo lifanywe kwa umakini.

Lusinde alinukuliwa akiwatetea wabunge hao akisema baadhi yao hawapo bungeni kwa vile wapo watu wanaoyashambulia majimbo yao kwa malengo ya 2015.

Alisema baadhi ya wanaoshambulia majimbo hayo ni makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya na mikoa, hivyo wabunge hao hawawezi kutulia bungeni wakati majimboni kunawaka moto.

Hoja hiyo ya Mhagama iliibua maswali mengi yasiyo na majibu kutoka kwa baadhi ya wabunge waliosema CCM haina mamlaka ya kumwadhibu mjumbe isipokuwa Mwenyekiti wa Bunge.

“Huko ni kutapatapa. Kanuni za Bunge hili ziko wazi kama kuna mjumbe ana udhuru atalazimika kutoa taarifa kwa mwenyekiti siyo CCM au taasisi aliyoingia nayo,” alidokeza mbunge mmoja.

Kifungu Namba 15 (1)(4) cha Kanuni za Kudumu za Bunge hilo kinaeleza adhabu ya mjumbe asiyehudhuria vikao hatalipwa posho ya kikao na kama atakuwa tayari amelipwa atairudisha.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM iliwahi kuomba baraka za Kamati Kuu ya chama hicho ili iweze kuwachukulia hatua watovu wa nidhamu na kwamba ilipewa mamlaka hayo.

“Kwa hiyo wanaposema kwamba chama kitachukua hatua ni kwa maana hiyo, kwamba ‘caucus’ ya wabunge wa CCM ni sehemu ya chama kwa hiyo wanapochukua hatua zozote zile, ni hatua za kichama kwa sababu wana baraka za Kamati Kuu na ninakumbuka walipewa mamlaka hayo,” alisema Nnauye.

Utoro

Suala la wajumbe hao kutajwa kuchukuliwa hatua limekuja baada ya Kamati za Bunge Maalumu kukamilisha uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, katika vikao ambavyo vilifanyika katika mazingira magumu kutokana na akidi kutotimia mara kadhaa.

Baadhi ya kamati zililazimika kuahirisha vikao na nyingine kuahirisha upigaji kura, kutokana na idadi ya wajumbe wanaotakiwa kutotimia, wajumbe wengine wakiwa ni makada wa CCM.

Uchache wa wajumbe unatokana na wajumbe ambao ni wanachama wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge hilo tangu Aprili 16, mwaka huu kutokana na kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda.

Mara kadhaa CCM kupitia vikao vyake mbalimbali ikiwamo Kamati Kuu (CC) iliyoketi takribani wiki mbili zilizopita, imekuwa ikitoa mwito kwa wabunge wake kushiriki vikao vya Bunge hilo.

Baadhi ya wajumbe wanaotajwa kutoshiriki ipasavyo ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye alisema amepata ruhusa ya Bunge.

Wengine wanaotajwa katika orodha hiyo na majimbo yao kwenye mabano ni Mohamed Dewji (Singida Mjini), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), Deo Filikunjombe (Ludewa), Kangi Lugola (Mwibara), Balozi Khamis Kagasheki (Bukoba Mjini) na Nimrodi Mkono (Musoma Vijijini).

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka ambaye ni miongoni mwa wabunge wanaotakiwa kulimwa barua, alijitetea katika kikao hicho kuwa alikuwa akiuguliwa.

“Kutokuwapo na kutoiongoza kamati kwa muda mrefu hakunizuii kusoma taarifa ya kamati yangu,” alisema Kilango.

Filikunjombe na Lugola walipoulizwa kwa nyakati tofauti kuhusu madai hayo, walisema wasingeweza kuzungumza kwa kuwa walikuwa kwenye mkutano.

Ole Sendeka alipoulizwa jana alisema hajui kama yumo au hayumo kwa vile hajaiona orodha hiyo... “Sijui kama nipo au simo katika hao wabunge 25 kwa sababu sijaiona hiyo orodha, ila ninachojua ni kwamba taarifa zangu wanazo sasa kama wataamua kuniandikia barua huku wakiwa na taarifa zangu basi tutajua huko mbele ya safari.”

Kabla ya kuwasilisha taarifa ya Kamati Namba 11 jana, Kilango ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, aliwapongeza wajumbe wa kamati yake kwa kufanya kazi bila yeye kuwepo kwani alikuwa na dharura ya kitaaluma.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname