Emmanuel Okwi.
STRAIKA wa Yanga, Emmanuel Okwi, hataichezea timu yake katika
mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo Jumamosi dhidi ya Komorozine ya
Comoro baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kushikilia leseni yake.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni
kwamba CAF imeshikilia leseni hiyo kutokana na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kutuma nakala ya barua yao iliyokwenda Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa) kuomba ufafanuzi juu ya uhalali wa uhamisho wa
Okwi wa kuichezea Yanga.
Mmoja wa maofisa wa TFF, alisema jana Ijumaa kuwa
CAF imewapatia leseni za wachezaji wengine 25 kati ya majina 26
yaliyokuwa yametumwa na Yanga, huku leseni ya Okwi ikibaki Cairo, Misri.
“CAF wamesema kuwa wakipata ufafanuzi kutoka Fifa
watatuma leseni hiyo, lakini kwa sasa hawataki kuleta mkanganyiko
mwingine,” alisema ofisa wa TFF.
Mchezaji huyo ambaye awali alikuwa wa Simba, aliuzwa kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia.
Hata hivyo inadaiwa kuwa klabu hiyo haikuilipa
Simba na wala haikuwa ikimpa mshahara, jambo lililomfanya Okwi asuse na
kurejea kwao Uganda kabla ya kuruhusiwa na Fifa kwa muda kujiunga na
Villa ya Uganda kisha kuibukia Yanga.
No comments:
Post a Comment