27 January 2014

UFOO SARO AZUNGUMZA KWA MARA YA KWANZA TOKEA MKASA WAKE WA KUPIGWA RISASI,HAYA NDIYO ALIYOSEMA

 Ni mara ya kwanza Saro kuzungumza tukio hilo tangu aliporuhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu, MOI ya Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.Hakika @Ufoo Saro aliokoka kuuliwa mwaka jana mwishoni@
Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi, amefanya ibada na kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumponya.”

Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, Jimbo la Magharibi, Ufoo huku akitokwa na machozi na wakati mwingine kushindwa kuzungumza alisema: “Ni miujiza tu ya Mungu yeye kunifanya mimi kuwa hai leo.”
Mtangazaji huyo ambaye alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili, aliwashukuru watu wote waliomtia moyo, kumsaidia kipindi chote alichokuwa mgonjwa.
 
“Sina cha kuwalipa, ninawashukuru sana kwa wema wenu, pia kwa kuniombea. Mungu ni mkubwa na amenipigania, naendelea vizuri kwa sasa,” alisema na kuongeza:
 
“Mungu alinisimamia na nyinyi pia mliniombea, hakika sina budi kushukuru kwa kila jambo. Nitasoma zaburi ya 146 katika Biblia Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa kunisaidia.”
 
Ufoo alisema kuwa ameamua kumshukuru Mungu kwa sababu siyo watu wote wanaopata matatizo kama yake wanapona.
 
Mchungaji aliyeongoza misa hiyo iliyoanza saa 1 asubuhi hadi saa 5 asubuhi,Joseph Maseghe alisema Mungu hakupanga Ufoo afariki dunia kwa kupigwa risasi.
 
“Mungu bado anakuhitaji, hakupanga ndiyo maana upo nasi leo. Hautakiwi kulia huu ni mwanzo wa maisha yako mengine, usilie unachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema

1 comment:

  1. Mchungaji Maseghe, elewa kwamba kulia kwake hakuna maana hamshukuru Mungu bali anatoa bubujiko la moyo wenye shukrani za dhati kwa Mungu toka kina cha ndani cha moyo wake kwa matendo makuu Mungu ametenda. Kulia pia relief ya kile kilichosibu moyo wa mtu na kumfanya mtu ajerejee kwenye hali yake ya uimara. Ufoo ni halali alie kwa sababu hata kusimama mbele za Madhabahu ya Mungu si kitu cha mchezo. Tunalia kwa Mungu kama sehemu ya majuto ya mambo mengi mabaya yaliyotukumba.Chozi ni jutio na ni toba ya hali ya juu kabisa kujililia nafsi yako.Mungu akulinde na kukupa moyo wa ujasiri kuhakikisha unaongezeka imani zaidi katika hayo yaliyokutokea umjue zaidi Mungu.

    ReplyDelete

Comments system

Disqus Shortname