JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, limemkamata Saida Mohamed (30), mkazi wa Mwasonga Kigamboni,
akiwa na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa
Agosti 31, mwaka huu, katika eneo la Mwasonga, Kigamboni.
Alisema Saida alikamatwa na suruali
saba, mashati saba ya kombati, kofia 10, shati mbili nyepesi, fulana
mbili na kofia moja aina ya bareti, vyote vikiwa mali ya JWTZ.
Alisema mtuhumiwa huyo, alikuwa na begi moja la kuwekea nguo za jeshi, cheo kimoja cha Koplo na mikanda miwili ya kijeshi.
Alisema uchunguzi unaendelea juu ya mwanamke huyo ili kubaini sababu za kumiliki sare za jeshi, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine, polisi wamemkamata
Husein Mkondoa (25), mkazi wa Gongolamboto Mzambarauni, akiwa
anaendesha pikipiki huku akiwa amevaa nguo za kiraia na kofia ngumu ya
kijani yenye nembo ya Polisi.
Alisema polisi walimtilia mashaka na kumkamata mtuhumiwa na anaendelea kuhojiwa.
“Naomba kutoa onyo kwa watu wote wenye
silaha na sare za jeshi wazisalimishe kwa polisi au ofisi yoyote ya
Serikali, msako wa kuwakamata wahalifu utakuwa endelevu na tutaingia
nyumba hadi nyumba kuwatafuta wahalifu.
“Sambamba na operesheni hii, licha ya
kubadilisha uongozi katika kituo cha Polisi Ubungo, tumeamua kutupia
macho vitendo vya utapeli katika eneo la Ubungo Bus Terminal, ambalo
watu wengi wanajifanya askari.
“Licha ya hilo, tumeunda kikosi cha
kutumia video kamera na kamera za picha mnato ili kubaini na kuchukua
hatua na nyendo mbalimbali ili kujenga ushahidi wa wahalifu hao
wasiepuke mkono wa sheria,” alisema Kova.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi
linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kuchonga hati mbalimbali zinazotaka
kufanana na za Serikali.
Kamishina Kova, aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Shadrack Samwel (27) mkazi wa Mbagala Sabasaba na Mwangi Samwel
(38) mkazi wa Kimara Baruti.
Alisema watu hao, hawana ofisi maalumu
hivyo hufanya shughuli hiyo sehemu yoyote na ofisi zao kuu ni mkoba
pamoja na gari ambalo wanatembelea, lenye namba za usajili T 397 ADX
aina ya Crester.
“Watuhumiwa hawa, tuliwakuta na mihuri
27 ambayo ni ya Serikali na taasisi binafsi, mihuri ya mawakili wa
kujitegemea na wa serikalini, mhuri wa Jeshi pamoja na mhuri wa Serikali
za mitaa.
“Pia tumewakamata na nakala mbalimbali
za SUMATRA, ikiwemo karatasi za kukagulia magari, pleti namba za magari
pamoja na nakala mbalimbali za ofisi hiyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, polisi
wanawashikilia watu watano, akiwamo Enea Dawsoni, ambaye ni mfanyakazi
katika Kapuni ya Ndege ya Fast Jet, kwa jaribio la kutaka kupora fedha
kiasi cha Sh 60,000,000 katika Kampuni hiyo.
Alisema watuhumiwa hao walinaswa katika Mtaa wa Samora na iligundulika walikuwa wana mawasiliano ya simu.
“Baada ya kuwakamata watu hawa, Polisi
walielekea katika ofisi hizo na baada ya kufika walichukua simu ya
watuhumiwa hao na kuona ujumbe mfupi wa maneno, ulioeleza kuwa fedha
zipo karibu na chooni.
“Polisi walichukua simu ya wahalifu na
walipopiga simu hiyo iliyokuwa na mawasiliano na majambazi hao, simu
iliita kwa sauti kubwa ndani ya maungo ya mmoja kati ya watumishi wa
Fast Jet.
“Mtumishi Enea Dawson alikuwa ameficha
simu hiyo sehemu za siri katika nguo zake ambapo aliumbuka na
kugundulika kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na majambazi hao,”
alisema Kova
Source:Mtanzania

No comments:
Post a Comment