MAZISHI ya rasta mmoja maarufu kwa jina la Rasta Gido aliyekuwa
dereva wa bodaboda yameonekana kushika nafasi ya juu katika rekodi ya
marehemu wote waliozikwa Ifakara, Morogoro miaka ya karibuni.
Rasta Gido alipata ajali mbaya ya kugongwa na gari aina ya Fuso, Julai 28, mwaka huu eneo la Ifakara Kibaoni.
Akizungumza na waandishi wetu juzi, jijini Dar baada ya kurejea
kutoka kwenye msiba huo, mjomba wa marehemu aitwaye Avi Simba alisema
msiba huo uliongozwa kwa imani ya kirasta bila kuhusisha mchungaji wala
shehe huku waombolezaji wakivalia kofia za kirasta zenye rangi za
kijani, nyekundu, njano na nyeusi hali iliyozidisha kuyafanya mazishi
hayo kuwa ya aina yake.
Mbali na kofia hizo, jeneza la marehemu lilipakwa rangi hizo za
kirasta zilizotajwa hapo juu, hivyo kulifanya eneo lote la msiba
kutawaliwa na taratibu za kirasta.
“Mimi na ndugu zangu wote tulikaa chini na kukubaliana kuwa marehemu
azikwe kwa imani ya kirasta bila kufuata taratibu za dini yoyote ile,”
alisema mjomba huyo wa marehemu.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wananchi waliohudhuria
msiba huo walijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na utaratibu wa
mazishi uliowekwa na ndugu na jamaa wa marehemu ambao ni jamii ya rasta
tofauti na taratibu za dini yake aliyokulia Rasta Gido ya Romani
Katoliki.
Hali iliyoongeza mazishi hayo kuwa ya aina yake ni Wazungu waliofika
msibani hapo sanjari na mwongozaji wa mazishi hayo, Rasta Side ambaye ni
mchumba wa mmoja wa Wazungu hao.
Mbali na hayo yote, kwenye mazishi, hakukutumika machepe na majembe
kufukia kaburi la marehemu huyo badala yake ilitumika mikono kufanya
kazi hiyo mwanzo hadi mwisho.
Kutokana na msiba huo, madereva wa bodaboda wa eneo la Kibaoni
waliamua kusitisha shughuli zao ili kuungana na mwenzao katika safari
yake ya mwisho.
Madereva hao walimlaani vikali dereva wa Fuso aliyemgonga Rasta Gido
wakidai kuwa hakuwa makini barabarani na kusababisha ajali hiyo mbaya.
Nayo familia ya marehemu ilijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na
jukumu zito la malezi alilowaachia rasta huyo kwani ameacha watoto
watatu, Rose, Neema na Stanislaus ambao wote bado wanahitaji msaada.
Marehemu Rasta Gido alizikwa kwenye makaburi ya familia ya Kibaoni, Ifakara mkoani Morogoro.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameni.

Blog yenu inakera unapofungua kusoma hbr inakua inafutika futika ndo nn sasa
ReplyDelete