Kijana Said Omari akionesha sehemu za vidole vyake vilivyoathirika kwa kemikali hizo
Na Mashaka Mhando,Handeni
VIJANA 12
wa kijiji cha Manga kilichopo kata ya Mkata wilayani hapa, wameanza
kunyofoka nyama kutokana na madai ya kubeba magunia yenye kemikali baada
ya lori lililokuwa limebeba mzigo huo, kupinduka katika eneo la dajani
la kitongoji cha Tengwe kijijini.
Vijana
hao wamepata athari hizo baada ya kupewa kibarua cha muda mfupi wa
kubeba maguni yaliyokuwa na uzito wa kilo 25 kuyafaulisha kwenye gari
jingine na kulipwa ujira wa sh. 95,000 ambazo waligawana sh. 11,500 kila
mmoja baada ya kumaliza kazi hiyo.
Ofisa
Tarafa ya Mazingara Bw Hashim Msagati alisema kuwa tukio hilo limetokea
Julai 26 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni katika eneo hilo baada ya
lori lenye namba za usajili T 787 CBT lililokuwa na tela lenye namba T
101 BTB kupinduka kisha watu waliokuwa kwenye gari hilo, kuwapa kazi
vijana hao kubeba mizigo hiyo.
Alisema
lori linadaiwa kumilikiwa na kiwanda cha soda cha Bonite kilichopo mjini
Moshi, lilipata ajali hiyo iliyothibitishwa na polisi wa kituo cha
Mkata, lilikuwa likitokea Jijini Dar es salaam kwenda mkoani
Kilimanjaro, likiwa limebeba mifuko yenye kemikali hizo.
Wakizungumza
na gazeti hili, wakiwa nyumbani kwao katika kijiji hicho cha Manga,
mmoja ya waathirika hao Bw. Said Omari alisema walipata kazi hiyo kutoka
kwa mtu mmoja aliyekuwa na asili ya Kihindi kupakia mifuko hiyo bila
kuelezwa kwamba kilichomo ndani yake ni madawa makali.
Aliwataja
wenzake waliokuwa pamoja ni Omari Bahorela, Khatib Juma, kassim Bakari,
Hamis Chilo, Ramadhani Rajab, Ramadhani Mbelwa na Omari Mbuji kutoka
katika mji wa Manga na Lazaro Jackson, Aweso Mussa, Mkombozi Mussa na
Mohamedi Shabani waliotokea kitongoji cha Tengwe.
Alisema
baada ya kufika kwenye eneo hilo, walianza kubeba mizigo hiyo na
kuipakia kwenye gari jingine lakini ghafla mwezao mmoja Kasimu alianza
kuanguka chini akawa hawezi kusimama baada ya madawa hayo kuanza
kumuunguza miguuni na kwenye shingo hatua ambayo walianza kuogopa
kuendelea na zoezi hilo.
"Mwenzetu
alipokuwa ameanguka chini akawa hawezi kuinuka huku akilia miguu
kumchoma kwa ndani na huku akishindwa kuinuka pale chini, tulianza
kuogopa tukamwagia maji tukazidisha maumivu, tulikataa kuendelea na
zoezi lile lakini yule Mhindi akasema hapana endeleeni mifuko iliyobaki,
vinginevyo hatatulipa," alisema Bw Said.
Alisema
hata hivyo, waliendelea kubeba na walipomaliza wakalipwa fedha hiyo
ingawa walikuwa wamekubaliana ujira wa sh. 100,000 wakapewa sh. 95,000,
lakini mwenzao yule hakuweza kutembea hadi wakambeba pamoja na Mhindi
huyo kumrudisha nyumbani kwao kisha wakaondoka kuendelea na safari.
Bw Said
alisema kesho yake walianza kunyofoka nyama kila mmoja aliyebeba mizigo
hiyo na ngozi kuwa nyeupe huku wakipata maumivu kwenye uti wa mgongo na
maeneo mengine ya miili yao hatua ambayo wanashindwa kupata matibabu
sahihi kutokana na kukosa fedha.
Akizungumzia
zaidi tukio hilo Bw. Msagati alisema kuwa wamepeleka taarifa hizo kwa
viongozi wa wilaya ili waweze kuchukua hatua ya kuwatafuta waliohusika
kwa ajili ya kuwasaidia matibabu vijana hao na kusafisha eneo lililopata
ajali hiyo amba[po wanahofu kwamba endapo mvua itanyesha, inaweza
kusombwa na kuingia katika visima vya maji na kuleta madhara makubwa kwa
jamii.
Mkuu wa
wilaya ya Handeni, Bw Muhingo Rweyemamu alisema atafika katika kijiji
hicho kuwatembelea vijana hao kisha kuona eneo lililopata ajali kabla ya
kuchukua hatua nyingine.
No comments:
Post a Comment