30 July 2013

HAWA NDO WANAWAKE KUMI BONGO WENYE VYEO VIKUBWA

Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro.
WANAWAKE wengi nchini wameshika vyeo mbalimbali vya juu serikali au kwenye taasisi binafsi. Wafuatao ni wanawake 10 ambao wanakalia au wamekalia vyeo hivyo hapa nchini kama walivyomulikwa na Elvan Stambuli.
JULIET  KARIUKI
HUYU ni Mkuruggenzi Mtendaji wa kwanza mwanamke katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) . Uteuzi wake ulifanywa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 12 mwaka huu na akakabidhiwa ofisi siku hiyohiyo.
Bibi Kariuki ana shahada ya kwanza ya sheria na ya uzamili, kwenye sheria ni mtalamu wa ubia kati ya serikali na watu binafsi (Public Private Partnership). Aliwahi kufanya kazi katika Chama Cha Mabenki ya Afrika Kusini.
MIZINGA MELU
NI  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC tangu  Machi 20 mwaka huu. Alichukua nafasi hiyo kutoka kwa  Lawrance Mafuru. Ni mzaliwa wa  Zambia katika Kijiji cha Mazabuka na ana shahada ya juu ya biashara (MBA), Zambia National Commercial Bank na Standard Chartered Bank.
SAUDA S. RAJABU
NAYE ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa juu wa Mkurugenzi Mkuu na Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Ndege ya Precision Air hapa nchini. Alianza kutumikia nafasi hiyo Machi Mosi, mwaka huu baada ya aliyekuwa akikalia kiti hicho, Alfonce Kioko kumaliza muda wake.
Ana shahada ya kwanza ya biashara na sasa yupo mbioni ‘kuchimbua’ shahada ya juu ya biashara. Amewahi kufanya kazi katika mashirika mengine ya ndege kama vile Kenya Airways na ya Rwanda na Burundi.
ANNE MAKINDA
NI mwanamke wa kwanza nchini kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Samwel Sitta ambaye aliliendesha Bunge kwa msimu mmoja tu mwaka 2005 hadi 2010.
Makinda amevunja rekodi kwa kukaa bungeni kwa miaka mingi kwani alianza kuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe mwaka 1975 hadi leo. Tayari ametangaza kung’atuka (2015).
BALOZI LIBERATA MULAMULA
NI Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico. Amewahi kuwa balozi wetu nchini Canada kuanzia mwaka 1999 hadi 2002. Amewahi kuteuliwa kuwa mmoja wa wasuluhishi wa mgogoro wa Rwanda. Ni msomi mwenye shahada ya kwanza na ya pili ya sanaa,alisomea Chuo Kikuu cha St. John’s, Marekani, 1989. (Pichani akiwa na Rais Obama.)
MCHUNGAJI G.RWAKATARE
HUYU ni Mchungaji na kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God na mwanzilishi wa shule za  St. Mary’s International alizozifungua mwaka 1997.
Licha ya kazi ya kuhubiri Injili, Mama Rwakatare ana chombo cha habari ambacho ni
Praise Power Radio 99.2 FM inayoelimisha jamii na kutoa burudani za kiroho.
GETRUDE MONGELLA
ALIKUWA mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Bunge la Afrika, amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini India 1991 hadi 1992 na akawa Katibu Mkuu katika Mkutano wa Wanawake Duniani uliofanyika Beijing, China  mwaka 1995.
Aliwahi kuwa mshauri wa Mkurugenzi Mkuu wa Unesco na aliwatumikia wananchi wa Ukerewe akiwa ni mbunge kuanzia 2000 hadi 2010 na Februari mwaka 2008 alikuwa  Mwenyekiti wa Bodi ya African Press Organization (APO).
ASHA ROSE MIGIRO
Asha-Rose Mtengeti Migiro ni mwanasheria na mwanasiasa. Licha ya kufundisha sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mama huyu aliwahi kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania. Lakini kikubwa zaidi ni pale alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Juni 2012. Baada ya kumaliza muda wake Umoja wa Mataifa, Migiro hivi sasa yupo nchini akiongoza kitengo cha Mambo ya Nchi za Nje cha Chama Cha Mapinduzi.
SUSAN MASHIBE
HUYU ni rubani na ni injinia wa ndege, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza nchini kuwa na elimu hizo alizopatia Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani. Ni Mwanzilishi na kiongozi wa Tanzanite Jet Centre Ltd, kampuni aliyoianzisha mwaka 2003 ambayo sasa inajulikana kama  Via Aviation  na inajishughulisha na biashara ya mambo ya anga nchini na barani Afrika. Alikutana na Rais Barrack Obama alipokuja nchini hivi karibuni.
JOYCE MHAVILE
NI Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One kuanzia 1994. Amekiongoza kituo hicho cha runinga hadi kushika nafasi ya kwanza kwa ufanisi mwaka jana.
Amebobea kwenye taaluma ya uandishi wa habari.  Ni mmoja wa wanawake katika Bara la Afrika walioongoza chombo cha habari kwa mafanikio na kuwa mfano kwa wasichana wanaochipukia hivi sasa katika nchi yetu.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname