YANGA imethibitisha kwamba kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet, atatua nchini kesho Jumapili tayari kusaini mkataba na kuanza kazi rasmi Jangwani.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 39, amewahi kuwa bosi wa Namibia, Zimbabwe, Ethiopia na Mkurugenzi wa Ufundi wa Nigeria.
Kiongozi wa Usajili wa Yanga, Seif Ahmed, aliiambia Mwanaspoti jana akisema: "Tumeshamalizana naye na atatua Jumapili, tutawatangazia mashabiki utaratibu wa mapokezi wakati wa mechi
yetu na Express (ya leo Jumamosi) lakini kimsingi kila kitu kimekamilika na wiki ijayo ataanza kazi baada ya kusaini mkataba.
"Tunataka awe na timu kabla ya mashindano ya Kagame kuanza ili aweze kuzoeana na wachezaji na kuijua timu vizuri."
Lakini ni wazi Kocha Msaidizi, Fred Minziro, ndiye atakayekuwa na kikosi muda mrefu kwani Tom atakuwa akiwasoma wachezaji.
Kocha huyo ana leseni ya kufundisha soka ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) aliyoipata mwaka 2000.
Kati ya mwaka 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Emmen inayocheza Ligi Daraja la Kwanza Uholanzi.
Pia amefanya kazi za uchambuzi wa soka katika televisheni za Ubelgiji, Afrika Kusini na Namibia.
Kocha huyo ambaye amesomea saikolojia na uchumi, anazungumza lugha nane za Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Faroe, Kiarabu, Kiafrikaan na Kihispania.
chanzo mwanasport
No comments:
Post a Comment