22 January 2016
HIZI NDO Sababu Tatu Zilizomrejesha Mbwana Samatta DRC
Baada ya Mbwana Samatta kurejea katika klabu ya TP Mazembe badala ya kwenda Ulaya kujiunga na Genk ya Ubelgiji, meneja wa mchezaji huyo Jamal Kisongo ametoa sababu tatu za maamuzi hayo.
Baada ya kushinda tuzo yake ya mwanasoka bora kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Bara hilo, Samatta ambaye ni mshambuliaji wa TP Mazembe ya Congo DR na timu ya taifa, Taifa Stars alitarajiwa kusafiri kwenda Ulaya lakini safari yake ilikwama kufuatia klabu hiyo ya Ubelgiji kushindwa kuafikiana dau na mmiliki Moise Katumbi.
Genk walikuwa wanataka kumsajili Samatta kwa dau ambalo mmiliki huyo wa TP Mazembe hakuridhika nalo kwa madai kwamba bei hiyo hailipi.
Kisongo alisema baada ya Katumbi kuonekana kushikilia msimamo wake wa kutomruhusu Samatta kwenda Genk, ndipo akaamua kumshinikiza nyota huyo arudi kwenye klabu yake ili amalizie mkataba wake na baada ya hapo aondoke akiwa kama mchezaji huru.
“Hiyo ni sababu ya kwanza ambayo tunaona kwa kufanya hivyo Katumbi lazima atakataa kuona Samatta anaondoka klabuni hapo akiwa kama mchezaji huru, jambo ambalo halitompa faida mmiliki huyo,”alisema Kisongo.
Alisema sababu ya pili ni kitendo cha udhalilishaji kilichotokea hivi karibuni cha gazeti moja la udaku kuandika kwamba Samatta alifumwa hotelini akiwa na mwanamke, hivyo wameona ni vema kumpeleka Congo ili kuepusha madhara yatakayotokana na kuharibiwa kwa saikolojia yake kufuatia habari hizo za uzushi.
Alisema kitendo cha Samatta kuendelea kukaa nchini kingezidi kutoa mwanya kwa magazeti ya udaku kumchafua na hivyo kuzima kabisa ndoto zake za kusonga mbele.
Kisongo alisema sababu ya tatu ni kumfanya nyota huyo asikae bila ya kuwa na mazoezi, hivyo ni bora aende Congo kufanya mazoezi na wenzake huku Katumbi akiwa anatafakari nini cha kufanya juu yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment