Wakati
Serikali ikihaha kuandaa mwongozo kwa vyuo na shule binafsi za msingi na
sekondari ili kudhibiti viwango vya ada, hali ni tofauti kwenye shule
za kimataifa ambazo zinaonekana kama zinachuana kwa kuwa na ada kubwa.
Wakati ada ya
juu kwa shule zinazotumia Kiingereza kuanzia elimu ya msingi ni kati ya
Sh2 milioni na Sh3 milioni, ada ya shule za kimataifa zilizopo nchini
inafikia hadi Sh60 milioni mwa mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa
na Mwananchi kwenye shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam na baadhi
ya mikoa.
Uchunguzi huo
unaonyesha kuwa mwanafunzi wa chekechea hutakiwa kulipa hadi Sh35
milioni kwa mwaka na fedha hizo hulipwa kwa kutumia dola ya Marekani.
Baadhi ya
shule zinapokea wanafunzi wenye asili ya Asia, nyingine hupokea
wanafunzi kutoka nchi tofauti bila ya kubagua na ni dhahiri kuwa hata
wazazi wa watoto ni wale wa kipato kikubwa.
Shule nyingi
zinatumia Kiingereza katika kufundisha masomo yote darasani kwa mitalaa
ya kimataifa na walimu wa kigeni ambao wanalipwa mishahara kwa viwango
vya kimataifa.
Wanafunzi
wanaosoma katika shule hizo wanaishi mazingira tofauti na wanaosoma
katika shule za kawaida. Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa
kike wakiwa wamevaa kaptura, bukta na sketi zinazoacha wazi mapaja,
kufuga rasta huku wavulana wakiwa huru kufuga nywele, na kuvaa hereni
bila kubanwa na sheria.
Shule na ada ni balaa
Kwa
kuzingatia nyaraka za kujiunga na shule ya International School of
Tanganyika (IST) iliyoko Masaki, ada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na
wa pili wa chekechea ni Sh35.9 milioni; darasa la tatu hadi la tano ada
ni Sh 39.8 milioni na kwa wale wanaoingia darasa la sita, la saba na la
nane ni Sh46. 3 milioni huku darasa la tisa na la kumi ada ni Sh49.2
milioni.
Mchanganuo wa
ada kwa mwanafunzi anayeingia darasa la 11 na 12 ni Sh 59.4 milioni.
Mbali ya ada hiyo, mwanafunzi hutakiwa pia kulipiwa gharama za ujenzi,
ada ya dharura, fomu ya kujiunga shuleni pamoja na michango mingine
ambavyo jumla ni Sh 19.8 milioni.
Shule
nyingine ambayo tozo zake - ada na michango mingine – imefuata mkondo
huo Braeburn iliyoko barabara ya Bagamoyo, Africana. Ada ya mwanafunzi
wa chekechea ni Sh 12.7 milioni kwa mwaka.
Mwaka wa
kwanza na wa pili ambao ni sawa na darasa la kwanza na la pili hulipa
Sh19.3 milioni. Darasa la tatu hadi la sita Sh21.1 milioni na darasa la
saba hadi la tisa (sekondari) ni Sh25.4 milioni. Mwanafunzi anayejiunga
na shule ya msingi ya Readers Rabbit iliyoko Masaki hutakiwa kulipa
kiasi cha Sh24.1 milioni kwa mwaka.
Tamongsco
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya alitetea ada hizo.
“Zinatumia
mitalaa ya kimataifa ambayo Tanzania haina walimu wanaoweza kuitumia
katika kufundisha. Pia, walimu hao wanalipwa kwa mishahara ya viwango
vya kimataifa,” alisema
Nkonya ambaye
wanachama wake wanapambana na Serikali dhidi ya uamuzi wa kuweka ada
elekezi, alisema sababu nyingine za shule hizo kutoza ada kubwa ni
gharama kubwa za vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini ambavyo
hufikia Sh7 milioni kwa miaka miwili, na pia huduma zake.
“Gharama zake
lazima zitakuwa juu kuliko za kwetu. Kwa mfano, mwanafunzi wa shule za
kimataifa anatakiwa akaone Mlima Alps au Everest,” alisema.
Lakini lengo
la shule hizo kufundisha kwa kutumia mitalaa ya nje ni kuepuka
kuwavuruga wanafunzi wa mataifa mengine ambao tayari walishaanza kutumia
mitalaa hiyo.
Kadhalika,
Nkonya alisema shule hizo hazina madhara kwa wanafunzi wa Kitanzania
kwani wanajifunza tamaduni za kigeni na kuchangamana na mataifa mengine.
Sababu nyingine ya shule hizo kutoza ada kubwa alisema ni masomo ya ziada kama kuogelea (lazima), kareti na muziki.
Shule ya Aga
Khan Tanzania (AKES, T) iliyoko Upanga ni ya kimataifa na inafundisha
kwa kutumia mitaala ya Uingereza. Shule hii inatoza ada ya Sh 7.4
milioni kwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea na
mwaka wa tatu analipiwa Sh 8.2 milioni.
Darasa la
kwanza hadi la sita ada ni Sh 9.4 milioni; sekondari ambayo ni darasa la
saba hadi la tisa ada ni Sh 9.9 milioni. Kwa wanafunzi wa darasa la 10
hadi 11 ada ni Sh 10.4 milioni wakati kidato cha tano ni kati ya Sh
20milioni hadi Sh22 milioni kwa mwaka.
Kwa mujibu wa
uchunguzi huo, Shule ya Kimataifa ya St Constantine yenye sekondari na
msingi, inatoza ada ya Sh7 milioni kwa wanafunzi wa chekechea, wakati
darasa la kwanza na la pili ni Sh9.5 milioni kwa mwaka na darasa la tatu
ni Sh11.7 milioni.
Wanafunzi wa
darasa la nne ni Sh12 milioni, la tano (Sh13 milioni), la sita (Sh13.5
milioni) na darasa la saba ambayo ni masomo ya sekondari ada hupanda
hadi Sh19.2 milioni, huku darasa la nane na tisa (Sh19.4 milioni) na
kidato cha tano na sita ni Sh 21. 7 milioni.
Pia, fedha za dharura, chakula cha mchana na safari ambazo jumla yake ni Sh3.6 milioni.
Shule ya
Haven of Peace (Hopac) iliyoko Mbezi Beach, mwanafunzi wa msingi
hulipiwa Sh17.2 milioni na sekondari ni Sh20.5 milioni. Gharama nyingine
mbali ya ada ni fedha za usaili, ukarabati na ada ya maendeleo ambavyo
jumla yake ni Sh 4.9 milioni.
Nyaraka za
kujiunga na shule ya msingi Genesis iliyopo Masaki zinaonyesha ada ni
Sh6.3 milioni kwa wanafunzi wa chekechea ambao husoma kwa miaka mitatu.
Kwa darasa la kwanza hadi la sita, ada ni Sh8.8 milioni na darasa la
nane ni Sh9.4 milioni.
Shule ya
kimataifa ya Laureate iliyoko Mikocheni inashika nafasi ya nane kwa ada
kubwa kwani katika mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea mwanafunzi
hutozwa Sh3.5 milioni kwa mwaka. Wanaoingia elimu ya msingi hadi darasa
la sita hulipa Sh4.7 milioni.
Sekondari,
yaani darasa la saba hadi la tisa ada ni Sh5.6 milioni na darasa la 11
na 12 ni Sh6.6 milioni. Kidato cha tano na sita ni Sh7.6 milioni kwa
mwaka na kila mwanafunzi hulipia usafiri Sh1.7 milioni kwa mwaka.
Katika Shule
ya Academic International, ada imechanganuliwa kwenye mfumo wa mihula
mitatu ambayo mwanafunzi anaweza kuilipa kwa mafungu. Jumla ya ada hiyo
kwa mwaka wa kwanza kwa chekechea ni Sh3.4 milioni na kwa wa pili
hupungua hadi Sh2.8 milioni.
Wanaoingia
darasa la kwanza hadi la sita ada ni Sh2.7 milioni kwa mwaka na darasa
la saba hutakiwa kulipa Sh3 milioni. Mchanganuo wa ada kwa kidato cha
kwanza na cha pili ni Sh3.8 milioni, kidato cha tatu wasiosoma sayansi
ni Sh3.9 milioni na wa masomo ya sayansi hulipa Sh 4.1 milioni.
Kidato cha
nne wasiosoma mchepuo wa sayansi ni Sh4.6 milioni na wanaosoma sayansi
ni Sh5.1 milioni. Kwa masomo ya kidato cha tano wasiosoma sayansi ada ni
Sh5.7 milioni wakati wanaosoma sayansi ni Sh5.9 milioni.
Masomo ya
kidato cha sita kwa wanaosoma sayansi ada ni Sh5.9 milioni na wasiosoma
sayansi ni Sh6.2 milioni. Pamoja na ada hiyo, kila mwanafunzi ni lazima
alipe fedha ya usajili Sh550,000, fomu ya maombi Sh150,000 na usafiri
kwa kila mwanafunzi Sh1.1 milioni kwa mwaka.
Tozo za ada
kwa shule ya East Africa International ni nafuu ikilinganishwa na shule
nyingine za kimataifa zinazofundisha kwa kutumia mitalaa na mihtasari ya
Uingereza. Kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, ada ni Sh2.7 milioni na
shule za sekondari ni Sh3.0 milioni. Ada hii inajumuisha pia usafiri,
kuogelea, kifungua kinywa na fedha ya kujisajili.
Shule za Feza
International za chekechea, msingi na sekondari zilizoko Kawe,
Mikocheni, na Tegeta kwa wasichana na wavulana hutegemea ngazi ya elimu.
“Mtoto wa
shule ya msingi analipiwa Sh4 milioni kwa mwaka na yule anayeanza
sekondari analipia zaidi ya Sh7 milioni. Kwa shule ya msingi ada pekee
ni Sh2.9 milioni bila kuhusisha gharama nyingine kama chakula, malazi,
vifaa na usajili,” alieleza mmoja wa wazazi ambaye ana mtoto wake
anasoma moja ya shule hizo.
No comments:
Post a Comment