Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Picha zikichukuliwa.
Na Dotto MwaibaleCHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimetangaza ratiba ya uzinduzi
wa kampeni za uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika viwanja vya
Jangwani jijini Dar es Salaam.
Katibu Muenezi wa chama
hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Juma ‘Gadafi’ akizungumza na
waandishi wa habari ofisi kwake Dar es Salaam leo asubuhi, alisema
maandalizi yote ya uzinduzi huo tayari yamekamilika.
“Maandalizi yote tayari
yamekamilika na leo jukwaa kubwa la kukaa viongozi linafungwa na
tunategemea kuwa na watu wengi katika uzinduzi huo” alisema Gadafi.
Gadafi alisema kuanzia
saa tatu asubuhi watu kutoka sehemu mbalimbali na wapenzi wa chama hicho
wataanza kuwasili katika viwanja hivyo ambapo viongozi wastaafu wa
chama na serikali na wale waliopo kazini watafuatia na kisha watawasili
mgombea nafasi ya urais kupitia CCM Dk.John Magufuli na mgombea mwenza
wake Samia Hassan Suluhu na baadae Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete.
Alisema katika uzinduzi
huo wageni mbalimbali wamealikwa kutoka mikoa ya jirani na mabalozi
kadhaa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Gadafi alisema kuwa
wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo viongozi wa chama hicho wakiwemo
mgombea urais Dk.Magufuli na mgombea mwenza wake watahutubia wanachama
kuelezea sera za chama hicho na utekelezaji wa ilani ya CCM kuelekea
uchaguzi mkuu.
Gadafi alitumia nafasi
hiyo kuwaomba wananchi, wanaccm na makundi mengine kufika katika
uzinduzi huo ambapo kutakuwepo na vikundi mbalimbali vya burudani na
kufanyika kwa dua za madhehebu yote za kukiombea chama hicho kuelekea
uchaguzi mkuu kama inavyofanyika vipindi vyote wanapo zindua kampeni za
uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine
Gadafi amekemea vikali vitendo vya udhalilishaji kwa wanachama wake vya
kuzomewa na kuchaniwa nguzo zao wanapopita maeneo ya Kariakoo na Mwenge.
Alisema kila mwana chama
yeyote wa chama cha siasa ana haki ya kuvaa nguo za chama chake hivyo
kuwazomea wanachama wao ni kukiuka sheria ya nchi na inaweza kuleta
ugomvi pale upande wa pili utakapoamua nao kujibu mapigo.
“Napenda kuiomba
serikali ya mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu,
Suleiman Kova kukomesha vitendo hivyo dhidi ya wanachama wetu na kama
wanaona tunawakera wasubiri majibu yao baada ya uchaguzi kwani CCM
itachukua ushindi mapema huku wakibaki wakishangaa” alisema Gadafi.
(Imeandaliwa wa habari za jamii)
No comments:
Post a Comment