05 March 2015

Simba yazuia Nyota Watatu wa Yanga Kuongeza Mkataba






KATIKA kuhakikisha wanakiboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Klabu ya Simba imewazuia wachezaji watatu wa Yanga kuongeza mikataba mipya ya kuichezea timu hiyo inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba katika mkutano wao mkuu wa timu hiyo, uliofanyika kwenye Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam, walitaja kukosekana wachezaji wenye uzoefu kwenye kikosi chao, ndiyo sababu ya kufanya vibaya katika msimu huu wa ligi.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba, wachezaji hao watatu waliozuiwa kuongeza mikataba mipya Yanga ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, wote raia wa Rwanda na Said Bahanuzi.

Chanzo hicho kilisema wachezaji hao ambao wote mikataba yao imemalizika, tayari wameanza mazungumzo ya awali na Simba kuhakikisha wanawasajili ili kukiimarisha kikosi chao katika msimu ujao.
“Simba wameshaanza mazungumzo na wachezaji watatu wa Yanga ambao unaweza kusema kuwa wapo huru; Twite, Niyonzima na Bahanuzi ambaye anacheza kwa mkopo timu ya Polisi.

“Simba walifanya hivyo baada tu ya kusikia kuwa mikataba yao inakwisha.
“Hiyo yote wamefanya kwa ajili ya kuboresha kikosi chao kwa kuwa kocha wao amesema anataka wachezaji wenye uzoefu na hawa ni kati ya wale aliowataja,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo, alisema: “Taarifa hizo siyo za kweli, hizo ni tetesi tu, Simba bado hawajanifuata kwa ajili ya mazungumzo na kama kweli wanataka kunisajili, basi wanifuate na siyo kuongea pembeni kwa kuwa naruhusiwa kuongea na timu yoyote kwa sasa.”

Naye Twite alisema: “Kiukweli kabisa hao Simba hawajanifuata kwa ajili ya mazungumzo yoyote, mimi bado mchezaji halali wa Yanga mwenye mkataba unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, hayo mengine siyajui.”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname