Uvumi
wa kuwapo kwa watu wanaoteka nyara watoto kwa kutumia magari aina ya
Noah, umeleta mtafaruku katika shule saba za msingi Manispaa ya Temeke,
na kusababisha wazazi kuvamia shule hizo na kufungwa kwa muda.
Hata
hivyo, katika baadhi ya shule hizo kumeripotiwa kutokea vurugu kiasi
cha jeshi la polisi kuingilia kati kutawanya watu waliotaka kuvunja
mageti ya kuingilia kwenye shule hizo.
Taarifa
za kuwapo kwa matukio ya watoto kutekwa na watu wasiojulikana zilianza
kuenea wiki tatu zilizopita, ambapo shule zilizoathirika ni Chekeni
Mwasonga, Mikwambe, Rangi Tatu, Mchikichini, Charambe, Kiburugwa,
Jitihada na Mbagala Kuu.
Akizungumza
na NIPASHE Jumamosi, Afisa Elimu ya Msingi Manispaa ya Temeke, Honorina
Mumba, alisema uvumi huo siyo wa kweli na hawafahamu nani anahusika
kuusambaza na kwa madhumuni gani.
Alikiri
kwamba kazi ya utoaji huduma katika baadhi ya shule umekuwa mgumu baada
ya wanafunzi kutofika shuleni kufuatia wazazi wao kuwazuia wakihofia
usalama wa watoto wao.
MATUKIO YALIVYOJIRI
Mumba
alisema taarifa ya kuwapo kwa watu wanaoteka nyara zilianzia katika
Shule ya Msingi Mwasonga, ambapo ghafla zilisambaa kwa kasi kutoka shule
moja hadi nyingine kiasi ambacho sasa inakuwa ngumu kudhibiti.
Imearifiwa
katika matukio hayo kila shule kuna watoto kati ya wanne hadi sita
walitekwa nyara katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana
ambao wanatumia magari ya Noah kwa ajili ya kutimiza vitendo hivyo.
“Hata
mimi nashangaa uvumi huu unavyoenea kwa kasi na kusababisha kazi ya
utoaji elimu kuwa ngumu, tunajitahidi sana kuwaelimisha wazazi lakini
kila siku shule moja hadi nyingine inaathirika,” alisema.
Alisema
Uongozi wa Manispaa ya Temeke kwa sasa unashirikiana na walimu na Jeshi
la polisi, kuhakikisha wanajitahidi kutuliza taharuki katika shule
hizo.
WALIMU WAKIRI HALI NI MBAYA
Wakizungumza
na mwandishi wa gazeti hili, baadhi ya walimu na viongozi wa serikali
za mitaa, walisema hali imekuwa mbaya katika shule hizo baada ya
wanafunzi kutohudhuria masomo kufuatia wazazi wao kuwazuia.
Mwenyekiti
wa mtaa Rangitatu, Said Pazi, alisema toka siku ya Jumatatu ilipotokea
tukio hilo, hali imekuwa ya wasiwasi kwa wanafunzi hao, ambapo baadhi
yao wameshindwa kuhudhuria masomo kikamilifu.
Alisema
siku ya tukio, kulikuwa na wakati mgumu baada ya wazazi waliokuwa na
taharuki kuvamia shule hiyo na kutaka kuvunja geti kuu la kuingilia
ndani, kushinikiza wapewe watoto wao baada ya kusikia kuna wanafunzi
watatu wametekwa nyara.
“Nikiwa
hapa ofisini wananchi walikuja na kuniambia kuna watoto wametekwa,
lakini kila nikijaribu kuuliza mazingira ya tukio hilo, hakuna aliyeweza
kueleza kwa usahihi, hata hivyo idadi ya watu ilipozidi kuongezeka na
kuhatarisha amani ilibidi tuwaite polisi watusaidie,” alisema Pazi.
Kwa
upande wa shule ya msingi, Jitihada ilibidi ichukuliwe hatua ya
kufungwa shule kwa siku moja baada ya wazazi kuamua kuwachukua watoto
wao kwa nguvu na wengine kukimbia ovyo baada ya kuenea taarifa ya
kutekwa wanafunzi sita.
Mwalimu
Mkuu wa Shule hiyo, Odenary Mosha, alisema tukio hilo limetokea juzi
majira ya saa 4.30 asubuhi, wakati wanafunzi wakiwa mapumziko.
Alisema
walijaribu kuwatuliza wazazi hao, lakini ilishindikana baada ya kuanza
kuvamia madarasa kwa nia ya kuwatafuta watoto wao.
Hata
hivyo, Mosha alisema hakuna mwanafunzi aliyeripotiwa kupotea na hata
mzazi aliyefika kusema mtoto hajarudi nyumbani kwao. Mwalimu mkuu wa
Shule ya Msingi Kiburugwa, Mponda Shabani, alisema kwa ujumla wanafunzi
wake wote 3,400 wapo salama na hakuna taarifa yoyote ya kupotea miongoni
mwao.
Hata
hivyo, Afisa Elimu mama Mumba, aliwashauri wazazi kuacha kusikiliza
maneno ya mitaani na kueleza katika shule zote kunafanyika zoezi maalum
la utoaji wa elimu wa kujitambua kwa wanafunzi.
DC: SINA TAARIFA
Mkuu
wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alipotafutwa kwa kutumia simu yake
ya kiganjani, alisema bado hajapata taarifa kuhusu matukio hayo na
kwamba analifanyia kazi.
KAMANDA KIENYA: NI WANAFUNZI WATORO
Kamanda
Mkoa wa kipolisi wa Temeke, Kienya Kienya, akizungumzia suala hilo,
alisema jambo hilo limezushwa na baadhi ya wanafunzi wasiopenda shule
kwa lengo la kusababisha hofu kwa wenzao.
Alisema jumla ya shule nne eneo la Mbagala zimeathirika kwa siku mbili pekee.
Hata
hivyo, kamanda huyo alisema kwamba yupo mbioni kushirikisha vyombo vya
habari kuhakikisha uvumi huo unamalizika ili kuondoa usumbufu kwa
wanafunzi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment