07 January 2014

ZITTO KABWE ANENA MAZITO..ASEMA WAPINZANI WAKISHIKA DOLA HAMNA MTANZANIA ATAKAYEPONA


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ametoa kauli nzito, baada ya kusema viongozi wa vyama vya siasa wanaopekua mawasiliano ya raia ni hatari kwa nchi na kwamba wakishika dola, raia wao hawatapona.

Kauli ya Zitto imekuja siku moja tu baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, kuutangazia umma kuwa wamenasa mawasiliano ya siri yanayodaiwa kufanywa na Zitto. Zitto aliliambia MTANZANIA jana kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kwamba sheria za nchi zinazuia mtu kupekuliwa mawasiliano yake.

“Sheria za nchi zinazuia mtu kupekuliwa pekuliwa mawasiliano, haki ya faragha ni haki yangu ya msingi.

“Kama viongozi wa chama cha siasa cha upinzani wanafanya kazi ya kupekua mawasiliano ya raia na kujiona wanafanya sahihi, watu hao ni hatari kwa nchi, maana wakishika dola raia hawatapona. Mimi siwajali watu hawa, nawadharau,” alisema Zitto.

Akizungumzia uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, Zitto alisema chama kimefanya uamuzi wake.

“Chama kimefanya uamuzi wake na ni wajibu wao akina Kitila na Mwigamba kuona kama wanapaswa kukata rufaa au hapana,” aliongeza Zitto.

Aidha amesikitishwa na kauli ya Dk. Slaa kuzuia wanachama wake kushiriki mikutano yake ya kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kukosa busara.

“Kwangu mimi, uamuzi wa Katibu Mkuu kuzuia viongozi na wanachama kushiriki mikutano yangu nadhani ni kukosa busara na hekima, suala langu bado liko mahakamani, likitoka litarudi kwenye chama.

“Nasisitiza, kutangaza namna hii si sawa kabisa kwa mujibu wa misingi yote ya demokrasia,” alisema Zitto.

PROFESA BAREGU
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, alisema viongozi wa chama hicho wanapaswa kulinda kauli zao ili kuepuka mvuragano unaoweza kutokea wakati huu.

“Wakati huu ambao chama kimekuwa na mambo mengi, nawasihi viongozi kuchunga kauli zao ili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kujitokeza.

“Nimekuwa msuluhishi ndani ya chama, nakwambia ndani ya chama haiwezekani fikra moja ikaendelea kudumu, kwa msingi huo lazima watu watofautiane mtazamo, si kila jambo kupinga.

“Katika hali hii, msimamo wangu ni kwamba changamoto inayotukabili tupunguze makali ya maamuzi, kwa sababu Watanzania wengi wanakitegemea chama hiki.

“Hivi sasa Watanzania wanajiandaa kukikabidhi CHADEMA dola, ni wakati mzuri wa viongozi kufikiria maisha ya chama kwanza na baadaye ukweli wa mambo utajulikana,” alisema.

NDANI YA KAMATI KUU
Habari za uhakika zilizopatikana jana kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichomalizika juzi jijini Dar es Salaam, zinasema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, tangu jana amekuwa akifanya mikutano ya ndani na baadhi ya viongozi mkoani Arusha kama njia ya kujipanga.

Mkutano kati ya Mbowe na viongozi hao ulianza jana na unatarajiwa kumalizika Januari 11, mwaka huu, huku mkutano huo ukitafsiriwa na baadhi ya wana CHADEMA kama mpango wa ushindi katika uchaguzi wa ndani kwa kiongozi huyo.

Mkutano huo, umekuja siku mbili baada ya kumalizika kwa mkutano wa Kamati Kuu na kuwa umekusudia kuangalia kasoro zilizojitokeza ndani ya chama.

Lakini chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa baadhi ya wajumbe waliohudhuria CC, walitoa angalizo kwa viongozi wa ngazi za juu, akiwemo Mbowe na Dk. Slaa kuwa makini juu ya uamuzi wanaochukua.

Wajumbe hao ni pamoja na Profesa Baregu na Wakili maarufu nchini, Mabere Marando.

“Hili jambo la Zitto ni wazi limeonekana kuwachanganya viongozi wa chama, baadhi ya wajumbe wa CC walifika mahali wakawa wanamshambulia Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), eti yuko mstari wa mbele kupinga uamuzi wa kumvua uongozi Zitto ndani ya chama.

“Ila Profesa Baregu yeye aliamua kupasua jipu, pale aliposema chama hakipaswi kumtafuta mchawi, kwa vile Dk. Slaa ndiye tatizo kubwa kwa kusikiliza maelezo ya upande mmoja,” kilisema chanzo chetu.

Akijitetea mbele ya kikao hicho, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila, alisema hakuwahi kuomba wala kugombea ujumbe wa Kamati Kuu, lakini alishangazwa na hatua ya kutangazwa kama mjumbe wakati siku zote amekuwa mshauri tu.

“Dk. Kitila ni mtu wa aina yake, awali alifuatwa na viongozi wa ngazi za juu, akiwemo Dk. Slaa, Wilfred Lwakatare pamoja na Mbowe, wote wakimtaka akifika mbele ya kikao aombe radhi wajumbe ili asamehewe.

“Lakini alipofika aliendelea kushikilia msimamo wake na kusema yupo tayari kupambana kwa lolote, kwani uamuzi wa kumtangaza kuwa ni mjumbe umemharibia hadi kufikia hatua ya kuvuliwa uongozi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Kitila ni kiboko, alisema yupo tayari kupambana katika eneo lolote na hajali hata kama atafukuzwa kazi UDSM, kwani mkakati huo ulifanywa kwa makusudi kwa lengo la kumharibia.

“Kila wakati lilipokuwa likijitokeza jambo la Dk. Kitila kuitwa mjumbe wa CC, Dk. Slaa na Mbowe walikuwa mstari wa mbele kumtetea na kusema si mjumbe, bali ni mshauri, lakini ameshangazwa na hatua ya sasa ya viongozi hao kumuita mjumbe wa CC na kwamba hizo ni mbinu za kumharibia na kwa upande wake anaamini ataweza kufanya kazi sehemu yoyote ile,” kilisema chanzo chetu.

MARANDO, PROF. SAFARI
Nao wajumbe wawili wa CC ambao pia ni mawakili maarufu nchini, Mabere Marando na Profesa Abdalah Safari, wamepinga vikali taarifa zilizosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, zinazodai wamejiondoa katika chama hicho.

Taarifa hizo zinadai wajumbe hao waliamua kujiondoa baada ya kutoridhika na uamuzi wa kufukuzwa uanachama kwa Dk. Kitila na Mwigamba.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Marando alisema hajawahi kufikiria wala kuwa na nia ya kujiondoa uanachama ndani ya chama hicho kama watu walivyosambaza katika mitandao.

“Sijawahi kuongea na binadamu yeyote, akiwemo mama yangu mzazi na mke wangu, kwa kuwa wao ndio watu wangu wa karibu kama nataka kujitoa, CHADEMA hao wanaosambaza habari hizo watakuwa hawana akili timamu,” alisema Marando.

Alisema hawezi kupingana na uamuzi wa CC kwa vile yeye ni mjumbe wa kamati hiyo, hivyo uamuzi unaofikiwa katika vikao vyote vya kamati kisheria naye hushiriki.

Kwa upande wa Profesa Safari, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, alisema hajawahi kususia kikao chochote cha chama chake.

“Mimi nilikuwepo katika mkutano siku zote na uamuzi ule nimeukubali mia kwa mia, sina kinyongo na bado nipo kwenye chama, sina mpango wa kujiondoa, hayo maneno yanayosambazwa katika mitandao hayana msingi hata kidogo,” alisema Profesa Safari.


Taarifa hii imeandaliwa na waandishi , Kulwa Karedia, Aziza Masoud na Kulwa Mzee

>>MTANZANIA

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname