11 January 2014

Roberto Carlos awafunda Yanga Uturuki


 
BEKI wa zamani wa Brazil na Real Madrid, Roberto Carlos,  amekaa dakika chache na wachezaji wa Yanga mjini Antalya, Uturuki na kuwapa somo la maana.
Carlos yuko mjini hapa na timu yake ya Sivasspor FC inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki. Timu ya Carlos inafanya mazoezi kwenye uwanja mmoja na Yanga na pia inaishi hoteli ya Sueno ilipo Yanga.
Gwiji huyo anayeheshimika kwa mafanikio yake aliyoyapata akitumia mguu wa kushoto, alishituka baada ya kusikia Yanga inatoka Tanzania ambako aliwahi kufundisha Kocha Mbrazili, Marcio Maximo, ambaye yeye anamheshimu sana.
Carlos alipiga picha na wachezaji wa Yanga halafu baadaye yeye na timu yake wakaangalia mazoezi ya wana Jangwani hao kwa dakika kumi kisha akakaa nao na kuzungumza kidogo na kuwachangamkia.
“Nimefurahi sana kusikia kwamba mmetoka Tanzania alikokuwa anafundisha Maximo (kocha wa zamani wa Taifa Stars), ninamheshimu sana yule kocha,” aliwaambia wachezaji wa Yanga.
“Ni katika watu muhimu sana kwangu, wachezaji nimewafurahia mnavyocheza. Mnachotakiwa kufanya ni kuongeza juhudi mkitambua kwamba kila mmoja ana nafasi yake ya kuonekana.”
Kocha anayeiongoza Yanga kwa sasa, Boniface Mkwasa, alisema mazoezi ambayo kikosi chake imeyaanza jana Ijumaa, yatasaidia kuiweka timu katika hali nzuri na kuwa tayari kwa mashindano. Leo Jumamosi Yanga itacheza mechi ya kujipima nguvu na Ankara Sekerspor ya Ligi Daraja la Pili Uturuki

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname