“Wengi wetu tunaishi bila kujiuliza maswali kama; “Itakuwaje iwapo siku nitaamka nikiwa sina uwezo wa kuona tena? Hatujiulizi maswali kama haya kwa sababu tunavichukulia vitu muhimu kuwa vya kawaida tu.”
“Hata mimi nilikuwa mmoja kati ya watu hao hadi
Januari 2008, nilipopoteza uwezo wa kuona, mama yangu alikuja kuniamsha
lakini jibu langu lilikuwa; siwezi kuona, siwezi kuona,” anaanza
kusimulia Margareth.
Miaka sita iliyopita Margareth Maganga alikwenda
kulala akiwa binti mwenye afya njema na furaha tele, lakini asubuhi ya
siku iliyofuata aliamka akiwa na ulemavu wa kutooona. Kwa kijana wa umri
wa miaka 19 tu, lilikuwa ni tukio la kutisha, kukatisha tamaa na kutia
simanzi.
Ilikuwa Ijumaa ya Januari 11, 2008 mama yake
Margareth alipokwenda kumwamsha binti yake kwani alikuwa amelala hata
baada ya muda wake wa kawaida kuamka kuwa umepita.
“Mama aliingia chumbani kuniamsha na kuhoji kwa
nini nilikuwa nimelala mpaka muda huo, nilimwambia sijaamka kwa kuwa
bado ulikuwa usiku, mama aliniambia tayari ilikuwa ni saa mbili asubuhi.
Nilifikicha macho kutazama, lakini sikuona kitu...; Nilibaini kuwa
nimepoteza uwezo wa kuona,” anasema Margareth.
Binti huyu ambaye sasa ana umri wa miaka 25
anasema kuwa mwanzoni alipopoteza uwezo wa kuona alihisi dunia
imemwelemea kutokana na ukweli kwamba, alianza kuona matarajio yake ya
kuwa mwanasheria yamepotea.
“Kilikuwa kipindi cha mateso kwangu na familia
yangu, ingawa wao walijaribu kutoonyesha hofu ili kunipa nafuu. Lakini
maswali kutoka kwa rafiki na kuishi kwa kutegemea msaada kwa kila
ninalotaka kufanya, vilinifanya nikate tamaa,” anasema Margareth.
Anaongeza kuwa alikosa raha kila alipokumbuka kuwa
hawezi kutimiza ndoto zake, lakini alipiga moyo konde na kukubali hali
yake, ingawa haikuwa rahisi kwake ukilinganisha na ndoto alizokuwa nazo.
Safari gizani
Pamoja na kuwa katika kipindi kigumu cha maisha yake, Margareth ameandika kitabu kiitwacho A Journey Through Darkness ambacho anaelezea safari yake tangu alipopoteza uwezo wa kuona.
Katika kitabu hicho anasimulia jinsi alivyoanza
kupata maumivu makali akiwa nchini Taiwan katika Kongamano la Vijana
(World Youth Conference for Adventist Youth), alipoanza kupata homa
kali na maumivu ya misuli.
“Sikutaka kuonekana mgonjwa, nilijikaza. Hata
hivyo, nilizidiwa na wenzangu walinipeleka hospitali. Majibu yalionyesha
kuwa nina upungufu wa damu hivyo niliambiwa kuna aina mbili za matitabu
ya haraka; moja ilikuwa kuongezewa damu au kupewa vidonge ambavyo
vingetuliza maumivu kwa muda,” anasema
Ilimchukua siku mbili kufika kwao Musoma na huko alianza
kupatiwa matibabu, mpaka ilipofika Januari 11 alipoamka akiwa amepoteza
uwezo wa kuona.
“Baada ya vipimo katika Hospitali za Muhimbili na
CCBRT, daktari alishauri nipelekwe nje ya nchi kufanyiwa matibabu kwani
hapa uwezo wao ulikuwa umefikia mwisho. Wazazi wangu walifanya mpango
nikapelekwa Marekani, baada ya kufanyiwa operesheni nilianza kuona kwa
mbali,” anasema na kuongeza:
“Nilipoteza uwezo wa kuona kwa zaidi ya mwezi
mmoja, hivyo kuziona tena sura za familia yangu na ndugu zangu wengine,
ilikuwa furaha ingawa siyo uono mzuri kama ule wa zamani.”
Margareth anasema kuwa anaamini kupoteza uwezo wa
kuona siyo mwisho wa maisha, kwani ungekuwa ndiyo ukweli wenyewe,
asingeweza kusoma Shahada ya Sheria na kuandika kitabu kwani vyote
amevifanya.
“Kupoteza uwezo wa kufanya jambo lolote inaweza
kuwa mwanzo mpya katika maisha yako. Nimemaliza shahada yangu ya sheria
nchini Uingereza, nimeandika kitabu na kuanzisha Shirika lisilo la
kiserikali la kusaidia wenye uono hafifu na wasioona liitwalo; Hope For
The Blind ,” anasema na kuongeza:
Misaada kwa wengine
“Ninasaidia wenye matatizo kama yangu kwa kutoa
Sh2,500 katika kila pesa ya kitabu kimoja ninachouza na kuiingiza katika
mfuko. Ninasaidia kwenye elimu na matibabu kwa kutumia pesa za mfuko
huo.”
Margareth anasema kuwa anaamini kwamba watu wengi wanapoteza uwezo wa kuona kutokana na kukosa matibabu sahihi.
“Mimi ni mfano mzuri, kwani kama wazazi wangu
wasingeweza kunipeleka nje ya nchi, ina maana leo hii nisingekuwa na
uwezo wa kuona, ingawa sioni vizuri. Wengi wanakosa matibabu sahihi,”
anasema.
Anaongeza kuwa ipo haja kwa Serikali kuangalia
tena namna matibabu ya watu wasioona, kwani matatizo yao mengine
yanaweza kutatuliwa, lakini hospitali hazina vifaa vya kutosha na
wataalamu.
“Ipo haja ya kuwekeza katika huduma za macho.
Naamini siyo kila asiyeona yupo hivyo kwa sababu Mungu amempangia,
isipokuwa ni kwa kukosa matibabu sahihi. Serikali iweke nguvu katika
hili pia,” anasema Margareth.
Kuhusu elimu ya watu wasioona, Margareth anasema
kuwa ni muhimu Serikali, wadau na watu binafsi wawekeze katika
kuwasaidia kwani wengi bado wanasoma katika mazingira magumu
ukilinganisha na mahitaji yao.
“Wasioona wanahitaji kupata elimu sahihi na kwa wakati, ni vyema
wote kwa pamoja tukasaidiana kuboresha mazingira yao ya kusomea kwani
yaliyopo hivi sasa hayaridhishi hata kidogo, na inavyoonekana hayapewi
kipaumbele,” anasema Margareth.
Margareth Maganga alizaliwa mwaka 1988. Elimu yake
ya msingi na sekondari alipata nchini Kenya katika Shule za Kajiado na
‘The Kenya High School’, baadaye alipata Shahada ya Sheria katika Chuo
Kikuu cha Leeds, Uingereza.
Ni mtoto wa kike pekee katika familia ya Paschal Manganga yenye watoto wengine wa kiume wa watatu, Evarist, Raphael na Luckness.
Mbali na kuwa mwanaharakati wa kusaidia watu wenye
matatizo ya kuona, Margareth anasema kuwa ndoto zake ni kuwa Jaji kwa
kuwa anataka kutoa haki kwa wanaostahili.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment