06 October 2013

Wauzaji wa MIKANDA ya video bandia za shambulio la KIGAIDI nchini kenya watiwa mbaron


Inasemekana walikusanya picha kadha za mkasa wa Westgate kuwa filamu ya kuvutia.
TAMAA ya wafanyabiashara jijini Nairobi kuvuna kutokana na mkasa wa Westgate iliwaweka pabaya Alhamisi, walipokamatwa kwa kuuza kanda haramu za mkasa huo.Maafisa wa Bodi ya Filamu Kenya wakishirikiana na wale wa CID, walivamia maduka ya kuuza CD jijini Nairobi ambako wafanyabiashara walikuwa wakiuza kanda hizo kwa Sh100 kila moja. 
Afisa wa bodi hiyo ya filamu, Bw Lawrence Mudaida, alisema ni makosa kwa mtu yeyote kukusanya matukio ya Westgate kuwa filamu kwa kuwa inaonyesha picha ambazo zinaweza kuwadhuru watu.


“Mbali na kuwa ni makosa kujinufaisha kutokana na maafa yaliyowapata watu wengine, pia ni kinyume cha sheria za filamu ambazo hazijapigwa msasa na kuidhinishwa na bodi hii,” akasema.



Matukio ndani ya jumba la Westgate yalikuwa ya kusisimua mno, ambapo raia na maafisa wa usalama waliingia humo kuokoa mateka waliozuiliwa na wavamizi hao wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab.



Inaaminika ufyatulianaji risasi uliokuwepo ndio ulivutia wafanyabiashara kutengeza filamu hizo.



Kwenye kisa hicho cha Septemba 21, magaidi waliokisiwa kuwa kati ya 10 na 15 walivamia jumba la Westgate na kuua watu 67 na kujeruhi wengine 175. Kundi la Al Shabaab, ambalo lina makao nchini Somalia lilidai kutekeleza shambulizi hilo kupitia mtandao wake wa Twitter.



Kampuni inayomiliki mtandao huo ilifunga anwani ya kundi hilo mara kwa mara lakini liliendelea kutuma jumbe kuhusu shambulizi hilo.



Sh100,000



Ulimwengu wote pia ulifuatilia shambulizi hilo baya zaidi tangu mlipuko wa bomu katika ubalozi wa Amerika 1998, ambapo watu 213 waliuawa kwa sababu vyombo vya habari vya humu nchini na kimataifa vilipeperusha matukio moja kwa moja.



Wachanganuzi wamefananisha shambulizi hilo na utekaji nyara katika hoteli moja jijini Mumbai, India, mnamo 2008 iliyotembelewa na raia wa Ulaya ambapo magaidi wa Pakistani waliteka watu nyara na kuua watu 166.



Hapo jana, maafisa wa Bodi ya Filamu Kenya walivamia vibanda vya kibiashara katika barabara ya Ronald Ngala, jijini Nairobi, na kunasa nakala 50 za kanda za filamu kuhusu shambulizi hilo ambapo watu kadha walitiwa mbaroni.



Wakipatikana na hatia, washukiwa hao wanaweza kutozwa faini ya Sh100,000 au wafungwe jela miezi mitano au adhabu zote mbili.



Bw Mudaida alisema maafisa wa bodi hiyo watashirikiana na polisi kuwasaka watayarishaji wa filamu hiyo ya shambulizi la kigaidi katika jumba la Westgate

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname