Utafiti mpya umebaini kuwa,
Watanzania wanaongoza katika Afrika kwa kuwa na hofu ya kutendewa
matukio ya kihalifu katika nyumba zao kutokana na kupungua kwa usalama
hapa nchini.
Hayo yalibainika kwenye majibu ya
utafiti uliotolewa jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Utafiti
kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), ambao unaonyesha kuwa asilimia 40 ya
wananchi 2,400 waliohojiwa wana hofu ya kufanyiwa uhalifu na kuifanya
Tanzania kuwa kinara kati ya nchi 34 zilizofanyiwa utafiti huo.
Nchi nyingine zilizopo katika tano bora ni; Afrika Kusini asilimia 38, Cameroon (37), Liberia (35) na Swaziland asilimia 34.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa kati ya Mei
hadi Juni, 2012, kwa kushirikiana na asasi ya Afrobarometer ililenga
kuchunguza hali ya uhalifu nchini na utayari wa wananchi kutoa taarifa
za kihalifu kwa polisi.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti
Msaidizi wa Repoa, Rose Aiko alisema kuwa vitendo vya watu kujeruhiwa
kutokana na uhalifu vimeongezeka nchini na idadi ya watu walzojeruhiwa
imeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2012.
“Utafiti unaonyesha kuwa matukio ya
mtu mmoja mmoja kupigwa na kujeruhiwa yameongezeka, huku wizi katika
nyumba nao umeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2005 hadi asilimia 36
mwaka 2012,” alisema Aiko.
Akifafanua namna ambavyo watu wana
hofu ya kuibiwa kwenye nyumba zao, Aiko alisema kuwa vitendo vya
kihalifu viliongezeka kuanzia mwaka 2008 na mwaka 2003 kulikuwa na
matukio mengi kwa asilimia 48, lakini mwaka 2005 yalipungua hadi kufikia
asilimia 34.
Hata hivyo, vitendo hivyo viliongezeka tena na kufikia asilimia 43 mwaka 2012.
Pia utafiti huo umebainisha kuwa
ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania ina
asilimia 32 ya watu waliowahi kuibiwa nyumbani, huku ikiwa na asilimia
26 ya watu hao katika Afrika.
Imebainika kuwa, asilimia 42 ya watu
waliofanyiwa vitendo vya kihalifu kati ya mwaka 2011 na 2012, ndiyo
waliotoa taarifa polisi huku ikielezwa kwamba wanaume ndiyo wanaoongoza
kwa kutoa taarifa hizo polisi.
“Utafiti unaonyesha kuwa wanawake ni
waoga zaidi wa matukio ya kihalifu ingawa imebainika kuwa sio wengi
wanaokumbwa na matukio hayo. Hata hivyo, imebainika kuwa wengi wapo
tayari kuripoti polisi taarifa za kuibiwa kuliko kupigwa,” ilisema
sehemu ya ripoti hiyo.
Mtafiti Mwandamizi wa Repoa, Dk Abel
Kinyondo alisema kuwa asilimia 18 ya waliohojiwa walisema hawakupeleka
taarifa za uhalifu polisi kwasababu vituo vipo mbali, asilimia 15
walisema polisi wana tabia ya kutokusilikiza shida zao, asilimia 14
walisema polisi wangetaka rushwa huku asilimia 12 walisema walitoa
taarifa kwa viongozi wengine walio karibu yao.
“Asilimia saba walisema hawana muda
wa kwenda kuripoti polisi, asilimia saba walisema waliogopa watu
waliowajeruhi wangeweza kuwatafuta tena wakati asilimia tano walisema
polisi wasingefanya chochote,” alisema Kinyondo.
Afisa Mnajimu Mipango na Bajeti,
Jeshi la Polisi, Beatus Silla alisema uelewa wa wananchi kuhusu namna
huduma za polisi zinavyoendeshwa umechangia baadhi yao kushindwa kwenda
polisi kutoa taarifa za kihalifu.
“Huduma za polisi ni bure, hakuna
gharama zozote na hilo tumelitangaza kwenye mabango katika vituo vya
polisi, namba za polisi pia zimetolewa ili kama mtu ana mashaka atoe
taarifa,” alisema Silla.
Akizungumzia malalamiko kuwa polisi
hawawajali wananchi wanapokwenda katika vituo kutoa taarifa mbalimbali,
Silla alisema: “Kuna dawati ambalo linashughulikia malalamiko kwa wadau
wa ndani ambao ni polisi wenyewe na wale wa nje ambao sisi tunawajibika
kwao.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa,
Profesa Samwel Wangwe alisema utafiti huo unaonyesha kuwa Tanzania ipo
katika wastani wa kati katika uhalifu Afrika, ingawa watu wengi
wameonyesha hofu na kutokuwa na amani na kushauri kufanyika marekebisho
katika Jeshi la Polisi.
“Kitaalamu inamaanisha kwamba,
tuangalie vizuri yale maboresho ya polisi na kwamba tufanye nini ili
yafanye kazi zaidi. Pili, utafiti wa sasa haukuingia ndani kueleza
kufanye nini na sababu ni nini,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Amoni
Chaligha kutoka Idara ya Siasa na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
alisema kuwa utafiti huo unapinga na hali ilivyo mitaani kwa kuwa zipo
baadhi ya nchi katika Afrika zinazofahamika kwa kuwa na kiwango kikubwa
cha uhalifu kuliko Tanzania, lakini ama hazipo au zimewekewa asilimia
ndogo.
“Sijui kwanini data zinaonyesha kuwa
ipo katika hali hiyo kwa sababu ukienda katika miji mingine kama
Johannesburg, Afrika Kusini hali ya uhalifu ni mbaya zaidi na hata
wakati wa Kombe la Dunia, 2010 ilielezwa zaidi hali hiyo, lakini
inashangaza kuona kama vile tupo sawa,” alisema Chaligha.
Chaligha alihoji pia: “Kinachowafanya watu kuwa na hofu ya uhalifu, ni kwa sababu wanasikia sana habari hizo kwenye vyombo mbalimbali vya habari?
No comments:
Post a Comment