NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kabwe Zitto amewaonya baadhi ya
wanasiasa wa vyama vya upinzani na chama tawala kuacha kumlazimisha Rais
Kikwete kutekeleza maoni yao binafsi kuhusu Muswada wa Sheria
uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Marekebisho
ya Katiba ya mwaka 2011.
Badala yake amewataka wanasiasa kuweka
mbele maslahi ya taifa kwa kutambua kuwa Katiba ni uhai wa Mtanzania
hivyo kurejea katika meza ya mazungumzo kwa pande zinazovutana kuhusu
nini kifanyike ili kuona namna ya kupata muafaka wa suala hili.
Zitto katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari aliyoitoa jana, alieleza kuwa ingawa kumekuwa na sintofahamu,
vuta nikuvute kuhusu muswada huo, bado kuna nafasi kama taifa kukaa na
kukubaliana na kuongeza kuwa kwa hali ilivyo nafasi hiyo ipo mikononi
mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
“Rais ana wajibu wa kikatiba wa
kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba
ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa
wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama
kutoridhia sheria hiyo.
“Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa
upinzani kujaribu kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama
chenye wabunge wengi bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati
huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri
hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo, kwani ni kinyume cha misingi
ya uongozi,” alisema Zitto.
Zitto alisema kwa takriban wiki tatu
sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada huo, jambo lililoweka
historia mbaya wakati wa mjadala wa suala hilo bungeni kulikochangiwa na
kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande zote mbili,
wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo jambo ambalo
halileti muafaka wa kitaifa.
Alisema masuala ya Tume imalize kazi
yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar
kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu wanapatikanaje na
kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka kwa viongozi kukaa
na kuzungumza.
“Haya sio masuala ya kushindwa kujenga
mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba
mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa. Ni
wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa
pasiwe na Katiba mpya ya wananchi,” alibainisha Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema.
Aidha, alisema lipo kundi lingine ambalo
lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka mingine zaidi
ili kuweza kupata kile kinachodhaniwa kuwa ni Katiba bora huku kundi la
Wabunge ambao chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi
uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge, jambo ambalo
halihusiani kabisa na kupata Katiba mpya. Zitto alikumbusha kuwa Chadema
iliwahi kupendekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya
sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na
kadhalika.
Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na
mapendekezo yao ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa
kuandika Katiba makini.
Alisema changamoto kubwa ya siasa za
Tanzania ni kelele ambapo alidai wanasiasa hawazungumzi masuala
yanayohusu uhai wa Taifa, bali kila chama kinakuwa na misimamo yake na
kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza na
kujadiliana kama Watanzania.
“Vyama vya upinzani nchini sasa
vimeungana kupinga muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya
Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi
ya Rais Mahusiano na Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao
wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo, badala ya kutafuta mwafaka,
kumekuwa na kurushiana maneno,” alieleza Zitto.
Alisema taifa linajengwa kwa mwafaka
hivyo alielekeza nafasi hiyo kwa Rais Kikwete kwamba atumie mamlaka yake
kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni
ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge.
“Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka
masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha
muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake
utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote”, alifafanua Zitto.
Naye Regina Kumba anaripoti kuwa
viongozi wa vyama vya upinzani wamekutana na msajili wa vyama vya Siasa,
Francis Mutungi na kumueleza sababu za kutaka Rais Jakaya Kikwete
asisaini muswada wa Mabadiliko ya katiba.
Aidha wamesema watashawishi wananchi
kupinga muswada huo iwapo rais atausaini. Viongozi hao wa CUF, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NCCR-Mageuzi, wamesema pia
walimueleza kilichotokea Bungeni Mkutano uliopita kwa wabunge wa vyama
vya upinzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
muda mfupi baada ya kukutana na msajili, Msemaji wa Chadema na Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika, alisema walikutana na Mutungi kwa nia ya kumueleza
nia yao.
“Tuliamua kuja kwa msajili kumueleza
kilichotufanya kuondoka katika Bunge lililopita na kwanini tumeamua sasa
kwenda kwa wananchi kufanya majadiliano baada ya yaliyotokea Bungeni
ili kupata hatima ya katiba yetu.”
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema ujio wao kwa msajili wa vyama vya siasa ni kumueleza
kilichojiri katika mchakato wa katiba ambao toka awali haukwenda vizuri
kutokana na ushiriki wa Zanzibar kuwa mdogo.
“Tumemjulisha kwa nini tumekuwa na
msimamo huu kuwa ikiendea kusainiwa rasimu hiyo kutakuwa hakuna maana ya
ushiriki wetu hivyo hatutashiriki tena kwa sababu Katiba ni ya
Watanzania na sio ya chama kimoja,” alisema Lipumba.
No comments:
Post a Comment