Wakati mwanamke wa kivazi kilichositisha ndoa kanisani kwa dakika kadhaa akidai hakuwa na tatizo kuvaa vile, Katekista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Peter, Yohane Maboko, amesisitiza kuwa alikiuka maadili ya Kanisa.
Mwanamke huyo ambaye ameendelea kukataa kutaja jina lake, huku njia zingine zikimtaja kwa jina la Restituta Kalemera, alidai jana kuwa kivazi hicho cha mabega wazi hakikuwa tatizo kanisani, bali ni unyanyasaji tu wa Katekista huyo.
Akizungumza jana, alidai kuwa Katekista Maboko alimsukuma na kumwangusha katika ngazi ndefu za Kanisa hilo lililoko Oysterbay, Dar es Salaam.
"Wakati Katekista akinitaka nitoke nje, ghafla alinisukuma nikaanguka kwenye ngazi na kudakwa na mtu mwingine aliyeniokoa, la sivyo ningeumia vibaya," alidai.
Alidai kilichomsikitisha ni kudaiwa kutaka kuingia kanisani akiwa amevaa nguo zilizoacha mwili wazi, jambo ambalo si la kweli, kwa kuwa alikwenda kanisani hapo akiwa na kitambaa kilichofunika mwili.
"Nilipofika kanisani, nilikutana na Katekista akimrudisha mtu mwingine, ghafla alitokea bibi harusi aliyevalia nguo ambazo hazikuruhusiwa kanisani, akaniomba skafu niliyokuwa nayo, nikampa nami kubaki wazi mabegani," alidai.
Baada ya kuvua kitambaa hicho, alidai alitaka kuingia kanisani ili kuchukua funguo za gari, lakini alikutana na Katekista kwenye ngazi, ambaye alimwamuru atoke nje naye akaendelea kumsihi kuwa anakwenda kuchukua funguo za gari ndani, hata hivyo hawakukubaliana.
Aliendelea kudai, kuwa Katekista alipomsukuma na kuanguka, baada ya kudakwa alichanganyikiwa akidhani kanisani ni sehemu ya malumbano, akakimbilia ndani kutafakari, huku kiatu chake alichonunua nje ya nchi (Uingereza) kikiwa kimeharibika.
Alidai kuwa akiwa kanisani, Katekista alimfuata tena na kumsihi atoke nje, jambo lililosababisha ndugu zake wamzingire kiongozi huyo wa Kanisa na kumhoji kwa jazba, sababu ya kumsukuma ndugu yao na kuhatarisha maisha yake.
Baada ya malumbano huyo, alitoka nje ya Kanisa na kuacha utaratibu mwingine ukiendelea, huku akilalamika kwamba Kanisa ni sehemu takatifu hivyo hapatakiwi kuwa uwanja wa mapigano na kwamba limeacha kazi ya kufundisha na kuomba ielezwe wazi watu wavae nini.
Akijibu tuhuma hizo, Katekista Maboko alimpongeza mwandishi kwa kushuhudia tukio hilo na kutoa habari yake na kuongeza kuwa utaratibu wa jinsi ya kuingia kanisani kwa maharusi, umekuwa ukifundishwa tangu kuandikishwa kwa ndoa hadi mafundisho ya ndoa.
Alisema dada huyo alipofika kanisani hapo, alikuwa na wanawe wawili waliokuwa na mavazi yaliyoacha sehemu za miili yao wazi, na aliwaelewesha lakini yeye akabisha.
"Niliwashika mikono na kuwapeleka uliko ubao ili wasome maelekezo ya kinachotakiwa kuvaliwa, lakini yeye alilazimisha kuingia huku akisema Mungu haangalii mavazi, bali roho," alisema Katekista Maboko na kuongeza kuwa wakati akieleza hayo, ndipo wanandugu walipofika na kumhoji.
Kuhusu miwani yake kuvunjwa, alisema wakati akiwa amezungukwa na watu kama 30 kwa lengo la kumchanganya, aliendelea kujenga hoja kuwa kanisani zipo taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa, lakini mmoja wao alitumia nguvu na kuvunja miwani hiyo.
Hata hivyo, alisema mtu huyo aliomba samahani na kulipa kiasi cha fedha, ambapo walipeana mikono kama ishara ya kusameheana.
Katekista Maboko alisema kwa ufupi kilichotokea, ni kukosekana kwa busara kwa waumini hao, kwani vipo vibao vinavyotoa maelekezo juu ya utaratibu unaotakiwa na unaopaswa kufuatwa.
No comments:
Post a Comment