Ili uweze kuwa na furaha maishani, lazima uwe katika uhusiano imara
usiotetereka. Kama unaishi na mke au mume ambaye moyo wako umemchagua
lazima furaha itatawala katika nyumba yenu. Lakini rafiki zangu, huwezi
kuwa katika ndoa yenye furaha kama hukuwa na mchumba bora. Kwa maneno
mengine, lazima uanze kuboresha uchumba wako kwanza, uwe na uhakika
kwamba mwenzi uliyenaye ni sahihi ili ukiingia kwenye ndoa usijute.
Mapenzi ni sawa na bustani nzuri ya maua rafiki zangu, wakati mwingine inahitaji mbolea, kumwagiliwa maji na hata kupaliliwa.
Kwa
kufanya hivyo utazidisha ladha ya mapenzi na kuyafanya yazidi kuwa na
nguvu zaidi ya awali. Lakini kama hutamwagilia, hutaweka mbolea,
hutapalilia, hesabu kwamba mapenzi yako yanaweza kuanza kupoteza nguvu
taratibu na hatimaye kufa kabisa.
Kikubwa ambacho nimepanga
kuzungumza nanyi leo ni jinsi ya kumpagawisha mwenzi wako ili awe wako
peke yako. Umeshawahi kufikiria kwamba, kama ukishindwa kutimiza mambo
fulani katika penzi au ndoa yako, mwenzi wako anaweza kuwa wa kushea?
Kama
bado, inakubidi ufahamu hilo kuanzia leo. Mpenzi anahitaji mambo mengi
ili aendelee kuwa mwaminifu kwenye penzi lenu. Ni kweli kwamba uaminifu
upo kwa mtu mwenyewe, kama mtu ni mwaminifu basi atadumisha uaminifu
uliopo ndani yake, lakini kama kuna mambo unakosea, lazima utasalitiwa!
Tena
basi, kama mwenzi wako anakupenda, atakusaliti huku analia! Kwanini?
Kwasababu analizwa ba kitendo ambacho hajapenda kukifanya ila wewe
mwenyewe ndiyo umemlazimisha afanye hivyo.
Kuna nini zaidi katika dhana ya usaliti?
Tukiachana
na tamaa, hulka na ushawishi, wakati mwingine mpenzi anaweza kusaliti
kwa kukosa yale ya muhimu zaidi katika penzi au ndoa yake.
Kwa
bahati mbaya sana, watu wa aina hii huwa hawasemi moja kwa moja kuwa
wanakosa vitu fulani au wanapenda vitu fulani, badala yake hutumia lugha
za ishara zaidi na kama hutaelewa basi huona suluhisho ni kutafuta
pumziko lingine.
Hapa sasa mwenzi wako anakuwa si wako peke yako
tena! Lakini lazima uhakikishe mpenzi wako anaendelea kuwa wako bila
kushea na mtu yeyote na jambo hili linawezekana kabisa ikiwa wewe
mwenyewe utataka iwe hivyo.
Zipo hatua au mambo mengi ya
kumfanyia mpenzi wako ili awe wako peke yako, lakini hapa nitakupa yale
ya msingi zaidi yatakayokusaidia katika penzi lako.
Njia hizi za
siri nimezifananisha na shamba au bustani, ambayo ina mahitaji yake.
Sasa katika uchambuzi huu, nitaainisha jinsi ya kuitunza bustani hii ya
mapenzi ili kuifanya bora zaidi kila siku.
Kitu cha kwanza kabisa
ni mbelea. Hapa nazungumzia penzi ambalo tayari limeshakuwa penzi! Kama
ni bustani basi tayari mboga zako zimemea vizuri.
Lakini ukumbuke kwamba, bustani yako haitaweza kuendelea kuwa bora kama haitakuwa na matunzo. Hapa penzi linahitaji mbolea.
Mbolea
ninayoizungumzia hapa ni maneno matamu yaliyojaa huba. Fikisha hisia
zako kwa mwenzi wako kwa namna ya kipekee iliyojaa penzi la dhati.
Mweleze
jinsi unavyompenda na jinsi maisha yako ambavyo hayawezi kukamilika
bila yeye. Huu ni wakati wako wa kumsumbua kwa meseji zilizojaa tungo za
mahaba, kadi, maua na zawadi ndogo ndogo.
Baadhi ya wanandoa
wakishaoana, huacha utaratibu huu. Kuna wanaosema: “Ah! Hayo mambo ya
kizamani bwana, kipindi akiwa demu wangu, sasa hivi yupo ndani, kwanini
nihangaike?”
Haya ni makosa makubwa ndugu yangu. Shamba bila mbolea kuna mavuno kweli? Huwezi kuvuna.
Kitu
kingine muhimu katika bustani, kama ujuavyo mpenzi msomaji wangu ni
maji. Bustani yako itahitaji maji kwa ajili ya kuzidisha ustawi wa mazao
yako. Hapa unatakiwa kuwa mbunifu zaidi katika mambo yanayohusu mapenzi
moja kwa moja.
Unatakiwa kubadilisha aina ya ufanywaji wa mapenzi,
mahali pa kukutana na hata sehemu za mitoko. Inashauriwa ili kuboresha
penzi ni vizuri kutoka sehemu mbalimbali na mwenzi wako. Inapendeza
zaidi angalau mara tatu kwa miezi sita, kulala na mwenzako hotelini.
Hapa utakuwa unanakshi zaidi penzi lako. Outing yako ni vyema ikawa ya kimahaba zaidi, kuanzia mavazi, sehemu mnazotembelea n.k
Mfanyie
mwenzi wako mambo ya kimahaba sana mnapokuwa wawili. Mbusu, mkumbatie,
mwambie jinsi unavyojisikia wa pekee kuwa wake. Utundu wako wote
umalizie hapa, ukifanya hivyo utakuwa umemwagilia bustani yako vyema.
Baada
ya muda bustani huota majani mengine ambayo si mboga! Yawezekana
kabisa, kwa bahati mbaya uchafu ukaingia bustanini. Wakati wa palizi ni
muda sahihi wa kuondoa vyote hivyo.
Hata katika mapenzi pia
hutakiwa kufanya jambo hili. Kugombana au kupishana kiswahili kwa
wapenzi ni jambo la kawaida sana, hivyo ni vyema kuweka sawa tofauti
hizo mapema, kabla tatizo halijawa kubwa zaidi. Hii ndiyo palizi
ninayoizungumzia.
Usikae na kinyongo moyoni mwako, kuwa mjanja,
hata kama ni yeye ndiye aliyekosea, zungumza naye ukimweleza jinsi
ambavyo hupendi mgombane, mkimweleza hisia zako kwamba unatamani sana
muelewane katika siku zote za maisha yenu. Weka mambo sawa.
Kwa
kufanya hivi, kwa hakika penzi lako litazidi kuwa imara zaidi na atakuwa
wako peke yako. Mapenzi ni utundu kidogo tu rafiki zangu. Nashukuru
sana kwa kunisoma, naweka kituo kikubwa.
No comments:
Post a Comment