WANAWAKE watatu raia wa Rwanda wanaosadikiwa kuendesha biashara ya ukahaba mjini Dodoma wamekamatwa na
kupewa siku tatu kuondoka nchini, huku wawili kati yao wakikutwa na vidonge vya kupunguza makali ya virusi ya Ukimwi (ARVs).
Kukamatwa kwa wanawake hao ambao ni Esperance
Hagenimana (28), Vestina
Zaninika (27) na Ziada Mukamurera (25), kunafuatia mmoja wao Esperance
kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kuwa alikuwa ameibiwa fedha
taslimu Sh 800,000 na hati ya kusafiria.
Lakini, Polisi walipofika nyumba ya kulala wageni waliyofikia iliyopo
eneo la Area D walikuta wanawake wengine wawili ambao walikuwa wakikaa
chumba kimoja na Esperance.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa mwanamke huyo hakuibiwa na kubaini
wote si raia wa Tanzania. Hata hivyo kilikosekana kifungu cha
kuwashitaki ndipo waliamua kupeleka sakata hilo Uhamiaji ili liweze
kushughulikiwa.
Kulingana na maelezo yao, Esperance alitangulia kuja nchini kisha
kuwaita wenzake ambao ilikuwa ni mara ya kwanza kuja nchini, lakini hata
hivyo alisema kuwa, kumekuwa na makundi ya wanawake kutoka Rwanda
wanaokuja nchini kipindi cha Bunge na hata mwaka jana kuna kundi
lilikuja wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Uhamiaji, wanawake hao waliingia
nchini na kujitambulisha kuwa walikuja Dodoma kufanya biashara ya
vitenge, lakini hawakuwa hata na kitenge kimoja ambacho kingeweza
kuwaonesha kuwa walikuwa wakifanya biashara hiyo.
Juhudi hizo za Uhamiaji zinadaiwa kuwafikisha hadi klabu moja maarufu ya
usiku iliyopo eneo la Area D ambapo walinzi wa Kimasai walikiri
kuwafahamu wanawake hao na walikuwa wakiwafuata nyumba ya wageni
waliyofikia kama mtu alikuwa akiwahitaji na walikuwa na ni wateja wa
klabu hiyo ya usiku.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Ofisa
Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Norah Massawe alikiri kukamatwa kwa wanawake
hao na polisi na kukabidhiwa Uhamiaji.
Alisema mwanzoni wanawake hao walidai kuwa walikuja Dodoma kwa ajili ya
kununua vitenge kwa ajili ya biashara na waliposhikiliwa na Polisi kwa
siku kadhaa waliomba kurudishwa nchini kwao.
Alisema wawili kati yao walikutwa wakiwa na vidonge vya ARVs, lakini haijafahamika moja kwa moja kama walikuwa wagonjwa au la.
“Siwezi kusema walikuwa ni makahaba bali wanahisiwa hivyo kutokana na
biashara waliyosema wanafanya kutoeleweka na hata maelezo ya walinzi wa
klabu ya usiku kuwa walitambuliwa kama wateja wao, kwa kweli hilo siwezi
kulithibitisha,” alisema.
Aliwataka wananchi kuwa makini na watu wasiowafahamu kwani hivi sasa
Mkoa wa Dodoma umekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu hasa katika kipindi
cha Bunge.
Mwandishi wa habari hizi, alimtafuta Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma,
Audrey Njelekela ambaye alisema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu kuanzia
ngazi ya Mkoa hadi mtaa ambapo kuna timu ya Mkoa ya Ukimwi na hata
kwenye halmashauri kuna waratibu ambao wamekuwa akitoa elimu juu ya
masuala mbalimbali yanayohusu Ukimwi.
Alisema kuwa kwa sasa kiwango cha maambukizi kwa Mkoa wa Dodoma ni
asilimia 2.9 kwa takwimu za mwaka 2011 na 2012 ikilinganisha na takwimu
za mwaka 2007 hadi 2008 ambapo kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia
3.3.
Alisema kuwa waratibu wa ngazi ya halmashauri wamekuwa wakitoa elimu juu
ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi kwenye maendeleo mbalimbali
ikiwemo klabu za usiku.
Alisema kwa kuwa kondomu zinasambazwa maeneo mbalimbali yakiwemo ya
starehe ni vyema wananchi kuhakikisha wanazitumia. “Matumizi ya kondomu
ni muhimu sana kwani maeneo ya klabu za usiku na maeneo mengine ya
starehe watu wengi wanachukuana tu lakini wanakuwa hawafahamiani,“
alisema.
Alisema kuwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika Mkoa wa Dodoma hasa kipindi cha Bunge, umakini zaidi unahitajika.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment