TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI UFAFANUZI KUHUSU SISI KUJIUNGA NA CHADEMA NA MALUMBANO KUHUSU MAJINA YETU
Tarehe
30/09/2012 mimi Esther Wasira na dada yangu Lilian Wasira tulijiunga na
CHADEMA na kukabidhiwa kadi na Katibu Mkuu wa CHADEMA Mh. Dr Willibrod
Slaa. Tulielezea kwa kirefu sababu za sisi kujiunga CHADEMA na
tukasisitiza kuwa tumeridhika
kuwa CHADEMA ni chama chenye dhamira safi
ya kuiongoza Tanzania na kwamba ni chama kinacholeta matumaini mapya ya
kuijenga Tanzania mpya yenye neema. Waandishi wa habari walijaribu
sana kutudodosa kujua tuna uhusiano gani na Waziri Steven Wasira.
Tulielezea wazi kuwa mahusiano yetu ya kifamilia hayahusiki na sababu na
dhamira yetu ya kujiunga CHADEMA. Hata hivyo tulielezea kuwa Waziri
Steven Wasira ni baba yetu mdogo ambaye alinyang'anyana ziwa na baba
yetu mzazi, wakili George Wasira. Tulidhani hiyo ilitosha na lisingekuwa
swala tena la kujadili na badala yake hoja ya kujadiliwa ingeweza kuwa
sababu tulizozieleza za kujiunga CHADEMA. Tunasikitishwa sana na
malumbano yaliyofuata baada ya hapo kuhusu kama sisi ni watoto wa Wasira
au la. Kama tulivyoeleza, tumejiunga CHADEMA kwa sababu tulizozieleza
hapo awali na wala si kwa sababu nyingine yeyote. Hatujajiunga CHADEMA
kumdhalilisha mtu, kumfedhehesha mtu au kukipatia umaarufu CHADEMA kwa
vile tu tunatumia jina la Wasira. CHADEMA ni chama cha siasa tena
chenye wanachama na wafuasi wengi Tanzania hivyo si kashfa bali ni
fahari kubwa mtu kujiunga CHADEMA na tena ni ushahidi wa mtu kujitambua.
Pia CHADEMA ni Chama maarufu sana Tanzania kwa sasa hata pengine ni
maarufu kuliko CCM hivyo hakihitaji kujipatia umaarufu kwa mgongo wetu.
Sisi tunawaheshimu sana wazee wetu na tutaendelea kuwaheshimu ila
linapokuja swala la chama cha kujiunga linabaki kuwa hiari yetu kwa
kuzingatia sera za chama na uwezo wa chama husika katika kujenga
Tanzania tunayoitaka na hilo ndilo lililotupeleka CHADEMA. Na hii ni
haki yetu ya msingi kabisa inayolindwa na Katiba ya nchi hii chini ya
ibara ya 20(1). Ikumbukwe kuwa mmoja wa Waanzilishi wa CHADEMA ni
Mzee Wasira. Dhamira ya kuanzisha CHADEMA ilikuwa ni kushika dola na
hili ndilo CHADEMA imekuwa siku zote inajaribu kuwashawishi Watanzania
kuwa sasa wamekomaa na wanastahili kuchukua dola. Kwa vile kuchukua dola
ilikuwa ndio ndoto ya baba yetu mzazi Mwanzilishi wa CHADEMA, sisi kama
watoto tumejiunga na M4C ya CHADEMA ili tuweze kutimiza ndoto ya baba
yetu kuwa CHADEMA siku moja ichukue jukumu la kuiongoza Tanzania.