20 October 2012

Dk Slaa ‘chali’ mahakamani

Dk Slaa ‘chali’ mahakamani

HATIMA ya ndoa ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na mpenzi wake, Josephine Mushumbusi imewekwa njia panda, baada ya mahakama kutupa pingamizi lake dhidi ya kesi iliyofunguliwa na Rose Kamili, ambaye anadai ndiye mke wake halali.
 Dk, Slaa na Josephine walitarajia kufunga ndoa kwenye Kanisa Katoliki Julai 21 mwaka huu, lakini Rose ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, alifungua kesi kupinga kufungwa kwa ndoa hiyo.

Na kwa upande wake, Dk Slaa pia kupitia kwa wakili wake, Phillemon Mutakyamirwa, aliweka pingamizi la awali dhidi ya Rose akidai kuwa hana haki ya kufungua kesi ya kupinga yeye kufunga ndoa na Josephine.

Pia aliiomba mahakama ifutilie mbali kesi hiyo.
Katika pingamizi hilo, Dk Slaa anadai kuwa hakuwa na ndoa halali na Rose na kwamba ndoa hiyo ni dhana tu, ambayo haiwezi kumfanya awe na nguvu ya kumpinga kufunga ndoa na Josephine.
Akitoa ufafanuzi wa pingamizi hilo, Wakili wake  (Mutakyamirwa) alisema kutokana na sababu hiyo, Rose hakupaswa kufungua kesi kupinga Dk Slaa kufunga ndoa na Josephine.

“Hakupaswa kuleta kufungua kesi ya kupinga kufungwa kwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kisheria, bali alipaswa kuleta maombi na hati ya kiapo, kuomba mahakama iangalie labda kama kuna mali walizochuma pamoja au matunzo ya watoto,” alisema Mutakyamirwa.
Hata hivyo Mahakama Kuu jana, ilitupilia mbali pingamizi la Dk Slaa, jambo ambalo limezidi kuiweka njia panda hatima ya ndoa hiyo.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo jana, Jaji Laurence Kaduri, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 160 (2) cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, mlalamikaji (Rose) ana haki ya kufungua madai hayo na kwamba mahakama ina mamlaka ya kuyasikiliza na kuyatolea uamuzi.

Jaji Kaduri alisema hata kama kulikuwa na ndoa ya dhana tu kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa, bado kifungu cha 160 (1) cha sheria hiyo kilichotumiwa na upande wa mlalamikaji katika pingamzi lao, bado hakimfungi mlalamikaji kufungua madai hayo.
“Kwa mtizamo wangu, ninaona kuwa mlalamikaji alikuwa sahihi kuleta madai haya, hivyo ninatupilia mbali pingamizi hili la awali.”, alisema Jaji Kaduri na kumtaka Dk Slaa kulipa gharama za uendeshaji wa pingamizi hilo.
Kutokana na pingamizi hilo la awali la Dk  Slaa kutupiliwa mbali, sasa mahakama itaendelea kusikiliza madai ya kesi ya msingi ya Rose na imepanga kesi hiyo kutajwa Desemba 6 mwaka huu.
Kama mahakama ingekubaliana na pingamizi la Dk Slaa, basi kesi iliyofunguliwa na Rose ingekuwa pia imeishia hapo na Dk Slaa angekuwa huru kufunga ndoa hiyo wakati wowote.
Hivyo, kutupiliwa mbali kwa pingamizi hilo kunazidi kuiweka njia panda hatima ya ndoa hiyo, kwa kuwa sasa itategemea uamuzi wa mahakama katika kesi ya msingi.

Wakati Dk Slaa akiweka pingamizi dhidi ya Rose kumfungulia kesi, Rose naye kupitia kwa wakili wake Joseph Tadayo aliweka pingamizi dhidi ya pingamizi la Dk Slaa.
Katika pingamizi lake, pamoja na mambo mengine, Rose alidai kuwa pingamizi hilo la Dk Slaa lina kasoro na kwamba limewasilishwa isivyo halali.
Kwa mujibu wa pingamizi hilo la Rose, pingamizi la Dk Slaa limewasilishwa mahakamani isivyohalali kwa kuwa halijathibitishwa kutokana na kutokuwapo kwa saini ya Josephine.
Hata hivyo mahakama iliamua kuanza kusikiliza pingamizi la Dk Slaa dhidi ya Rose na ikaamuru usikilizwajiwa huo ufanyike kwa njia ya maandishi, baada ya mawakili wa pande zote kukubaliana hivyo.

Source-mwananchi comm

Comments system

Disqus Shortname