Naibu
katibu mkuu wa CUF na Mjumbe wa Baraza la wawakilishi, Mh. Ismail Jussa
Ladhu, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya uongozi katika chama.
Ifuatayo ni taarifa iliyotolewa na Mh. Jussa kuhusu kujiuzulu kwake.
Leo asubuhi nimewasilisha kwa Mwenyekiti wa
Chama Taifa, Mheshimiwa
Profesa Ibrahim Lipumba barua ya kuomba kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Zanzibar, uamuzi ambao
nimeomba uanze kutekelezwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 2012.
Nimechukua uamuzi huu baada ya kuzungumza na kushauriana na viongozi
wangu wa juu wa Chama ambao ni Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu
Mwenyekiti Mheshimiwa Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif
Sharif Hamad takriban miezi miwili iliyopita. Nawashukuru baada ya
kunitaka niwape muda wa kulitafakari walinikubalia lakini wakaniomba
nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi ya shughuli muhimu za Chama katika
kipindi hichi.
Sababu kubwa zilizonisukuma kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi
hii ni kutokana na muda mrefu sasa kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya
kuwa msimamizi mkuu wa utendaji wa Chama kwa upande wa Zanzibar na
wakati huo huo kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji
Mkongwe hakunipi fursa ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote mbili kwa
ufanisi unaotakiwa. Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na nje
ya Baraza ili iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi.
Sambamba na sababu hiyo ni kwamba nimekusudia kutumia muda mwingi
zaidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika harakati za wananchi wa Zanzibar
zinazoendelea za kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake
kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa
Mkataba kati yake na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na
kimataifa.
Harakati zinazoendelea Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia
kwa kutumia mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa
msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na
wananchi wa Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao na ya nchi yao.
Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya kiutendaji
nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na Wawakilishi wenzangu
tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa vilivyomo Barazani.
Nafurahi kwamba leo nimetimiza azma yangu hiyo. Pamoja na uamuzi huu,
naendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. Nawahakikishia viongozi na wanachama
wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana pamoja katika shughuli
nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja tutafanya kazi
kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa ushirikiano kikamilifu
mwanachama yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi ninayoiwacha.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
Zanzibar
05 Oktoba, 2012