NI vigumu
kuamini kilichotokea lakini ndivyo ilivyokuwa! Mtoto Christian Alex (6)
ameuawa kikatili kwa kuliwa na mbwa wanaodaiwa kuwa ni wa Ubalozi wa
Qatar nchini Tanzania unaoongozwa na Balozi Jassim Mohammed Mubarak
Daruwesh.
Tukio
hilo la kusikitisha lilijiri Machi 26, mwaka huu Jangwani Beach,
Kunduchi jijini Dar es Salaam ambapo mtoto huyo alishambuliwa na mbwa wa
kigogo huyo alipokuwa na baba yake jirani na nyumba hiyo ya kupanga
yenye nyumba nyingine mbalimbali (apartment).
MAELEZO KWA UFUPI
Inaelezwa
kuwa, baba wa marehemu pia anaishi kwenye moja ya nyumba hizo akifanya
kazi ya kutunza mazingira endapo mpangaji mmoja anahama. Wote wanaoishi
humo wanatumia mageti mawili tu, kuingia na kutoka.
BABA WA MAREHEMU ASIMULIA
Akizungumza
na gazeti hili kwa majonzi kwenye msiba uliogubikwa na vilio na
simanzi, baba wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Alex, alisema
siku ya tukio yeye alikuwa akitoka nje ya nyumba anayoishi katika
‘apartment’ hizo, lakini ghafla nyuma yake alisikia kelele za mwanaye.
“Kwa
kawaida ili utoke lazima uwe makini, kwanza ujue mbwa wako wapi?
Nilipotoka nikiwa nawaangalia walipo, mara nikasikia kelele mtoto wangu
analia, nilirudi haraka, nikamkuta mwanangu anashambuliwa na mbwa watatu
huku tayari akiwa na majeraha makubwa.
“Ilibidi
nimng’ang’anie mtoto ili kumwokoa ambapo pia niliokota jiwe kutaka
kuwapiga, wakataka kuondoka lakini wakarudi tena na kumvamia.
“Hapo
ndipo ilikuwa shughuli kwani walimfumua utumbo, wakazinyofoa sehemu zake
za siri na kuziingiza midomoni huku kisogoni wakimtia kucha kali mpaka
kumtoa ngozi.
“Wakati
kitendo hicho kinaendelea huku nikishuhudia kwa macho, yule balozi akawa
anaingia ndani, akawaamuru mbwa wake waache, walitii amri hiyo lakini
hali ya mtoto wangu ilikuwa mbaya sana, akawa hasemi wala hapigi kelele
tena za kuomba msaada,” alisema baba huyo huku akimwaga machozi. Inauma
sana!
Akaongeza:
“Mpaka sasa siamini kilichotokea, nashindwa hata niongee nini,
ninachoweza kusema ni kwamba mwanangu Christian nilikuwa nampenda sana
kama vile ninavyompenda mwanangu mwingine, Sabina.
“Nahisi
ukiwa baada ya kupoteza mtoto wa kiume niliyekuwa namtegemea.
Itanichukua muda mrefu sana kusahau kile nilichokiona kwa macho yangu.
Nimeshuhudia mwanangu akishambuliwa na wala sikusimuliwa na mtu.”
Mazishi yakiendelea.
KUMBE TAHADHARI ILITOLEWA
Baba
anaendelea kusimuliza: “Kinachoniuma zaidi ni kwamba, nilishatoa
angalizo tangu mwanzoni wakati huyu bwana anahamia kwenye nyumba hii.
Nilimwambia mwenye nyumba amwambie huyu awajengee banda mbwa wake
lakini wakapuuzia.”
ADAKTARI WALIVYOSEMA
Baadhi ya
majirani walifika eneo la tukio na kukuta sakata hilo limefikia hatua
ya mbwa kutii amri ya bosi wao na kurudi kwenye maskani yao.
Walimchukua
mtoto huyo na kumkimbiza kwenye Hospitali ya IMTU iliyopo Mbezi, Dar
ambapo madaktari walisema alishafariki dunia kitambo.
VILIO VYATAWALA
Baada
ya kuzinyaka taarifa hizo, haraka mwandishi wetu alifika eneo la tukio
muda mfupi baada ya mtoto huyo kupelekwa hospitali na kushuhudia vilio
vikitawala kwa kila jirani aliyepata taarifa za kifo hicho cha
kusikitisha.
MAJIRANI WASIMULIA
Wakionesha
jinsi walivyoumizwa na tukio hilo, baadhi ya majirani walisimulia jinsi
mbwa hao wanavyowatishia amani katika nyumba hiyo ambapo tangu kigogo
huyo ahamie ndani ya nyumba hiyo wamekuwa watu wa kujifungia siku nzima
wakihofia mbwa hao wakali.
“Jamani
huyu mtoto kafa kifo kibaya sana, mbaya zaidi mbwa hawa wamekuwa tishio
kiasi cha watu kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.
“Mbwa huwa hawafungiwi kwenye banda, labda ingekuwa hivyo wasingefanya hivi,” alisema jirani mmoja huku akilia bila kikomo.
POLISI WALIVYOFANYA
Paparazi
wetu alipojaribu kuingia ndani na kwenda kuongea na balozi huyo, askari
waliodaiwa ni wa Kituo cha Polisi Kawe jijini Dar walitia ngumu huku
ikidaiwa kuwa maelezo waliyoyaandika ni mmiliki wa mbwa kuwa mzembe kwa
kuwaachia mbwa kudhuru binadamu.
MAMA MZAZI AZIMIA
Maria
Mvile, mama mzazi wa marehemu Christian kwa sasa yupo katika hali mbaya
tangu mkasa wa kushambuliwa mwanaye na mbwa hao utokee ambapo amekuwa
akizimia mara kwa mara.
Mwandishi wetu alimshuhudia mama huyo akishindwa kuweka shada la maua katika kaburi la mwanaye kwa kuanguka na kuzimia.
MAZIKO
Safari ya
mwisho ya mtoto Christian ilifanyika kwenye Makaburi ya Mburahati, Dar
es Salaam ikitanguliwa na misa iliyosomwa na Katekista wa Kanisa
Katoliki Mburahati, Owen Hokororo.
Kamanda wa
Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camillius Wambura amethibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kukiri kuwa ni nyumbani kwa balozi wa Qatar nchini.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment