17 February 2014

Wajumbe wa Bunge la Katiba kulipwa sh. 300,000 kwa siku na siyo sh. 700,000/= kama ilivyodaiwa hapo awali alifafanua katibu wa bunge


Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Thomas Kashillilah, amewaambia waandishi wa habari kuwa  Bunge Maalumu la Katiba litazinduliwa rasmi Februari 26, 2014 huku kila mjumbe akilipwa posho ya shilingi laki tatu na siyo shilingi laki saba kama ilivyochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari.
“Sisi tumesikia kuwa Wabunge wa Bunge la Katiba wanalipwa 700,000 na wala hatujui hili limetoka wapi, kwanza mamlaka ya kuidhibisha posho ni la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na hajaidhinisha Sh. 700,000.
Alisema Wajumbe watalipwa posho ya kawaida ya Serikali ya siku (hakuitaja), lakini alisema kutawakuwa na kodi maalumu ambayo itahusisha posho ya kikao, usafiri, malipo kwa madereva na mengineyo. Hivyo posho ya kawaida itakuwa Sh 80,000/=
“Kwa hiyo posho aliyoidhinisha ni posho inayolipwa sasa..kwa maana fedha ya kujikimu ni sawa sawa na viwango vingine, kwa maana posho ya kikao na posho ya usafiri imechanganywa kwa pamoja inalipwa kama ni posho ambayo ni ya kawaida ambayo ni Sh. 220,000. 
“Jumla Mbunge wa Bunge Maalum akija Dodoma akiingia kwenye kikao atalipwa Sh. 300,000”
Kashilillah alisema Bunge Maalumu litajumuisha wajumbe 629 ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 357, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) 82 na wajumbe wa kuteuliwa kwa uwakilishi 201.

Alisema kuwa katika idadi hiyo, punguza wajumbe sita wa Baraza la Wawakilishi ambao pia ni wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mjumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, wabunge wawili waliofariki na nafasi mbili za uteuzi wa Rais zilizo wazi, hivyo unapata wajumbe 629.

Amesema Bunge hilo litaanza kwa mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi kesho asubuhi na tayari utekelezaji wa ratiba umeanza jana kwa kusajili wajumbe --ambapo zaidi ya 120 walikwisha jisajili hadi kufikia jana mchana-- kazi ambayo itaendelea leo.

Amesema kesho saa 8 mchana, kutasomwa tangazo la kuitisha Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda na kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge hilo.
"Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Katibu wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao utaratibu tutatoa leo. Mwenyekiti wa Muda atasimamia kuchaguliwa kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba," 
alisema Dk Kashillilah.

Alisema Mwenyekiti wa Muda atakayechaguliwa Februari 21, pia atasimamia kuandaliwa kwa Kanuni, na baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, ndipo atateuliwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo kwa mujibu wa sheria kwani yeye na mwenzake wa Zanzibar kwa sasa wanasimamia tu mchakato huo.

Alisema kabla ya Mwenyekiti na Makamu wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kuanza kazi zao, kwanza watasubiri Rais kuwaapisha Katibu na Naibu Katibu, na ndipo Katibu wa Bunge hilo, atakuja kumwapisha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti; na Mwenyekiti kuwaapisha wajumbe wake.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumatano na Alhamisi zitatumika kwa kikao cha kazi cha kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, wakati Ijumaa itakuwa siku ya kupitisha Azimio la kuridhia Kanuni za Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na kiapo cha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu (ingawa hiyo siyo shughuli ya Bunge Maalumu).

Dk Kashillilah alisema Jumamosi, itakuwa ni kiapo cha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na kufuatiwa na kiapo cha wajumbe wa Bunge Maalumu ambacho kitaendelea hadi Jumapili.

Aidha, Jumatatu pia kutakuwa na kiapo cha wajumbe saa 4 asubuhi na kuunda Kamati za Bunge Maalumu, kabla ya ufunguzi rasmi wa Bunge utakaofanywa na Rais Jakaya Kikwete, saa 10 jioni.

Alisema pia kuwa uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu itakuwa ni Jumanne na Jumatano ya Februari 26, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba utaanza hadi Aprili 30, mwaka huu.
“Baada ya uzinduzi huo kufanywa ndiyo Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwa mpangilio tuliouanisha katika ratiba ambayo tutakuwa tumewapa... kwa hiyo baada ya pale Rasimu ikiwasilishwa na kanuni zitakuwa zimeainisha ni kwa utaratibu gani Rasimu hiyo kabla ya kuwasilishwa itajadiliwa hatua kwa hatua mpaka mwisho, ambapo sasa itakuwa imepatikana Katiba inayopendekezwa ili iende kwa wananchi kwa ajili ya kupata ridhaa,” 
alisema Dk. Kashilila.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa na kutunga masharti ya Mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalumu litakavyoona inafaa.

Ili Katiba inayopendekezwa ipitishwe katika Bunge Maalumu la Katiba, itahitajika kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, muda ambao Bunge Maalumu litajadili Rasimu ya Katiba hautazidi siku 70 kuanzia tarehe ambayo Bunge Maalumu lilipoitishwa, hivyo uhai wa Bunge hili unatarajiwa kukoma Aprili 30, mwaka huu, lakini unaweza kuongezwa kwa mashauriano kati ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na Makamu wake kwa ridhaa ya Rais kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.
 
UKARABATI ULIOGHARIMU BILIONI Sh8.2/= 
Akizungumzia gharama za ukarabati wa jengo na miundombinu mingine, Dk Kashillilah alisema ni Sh bilioni 8.2, ambazo zote zimetoka katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambayo ilishapitishwa na Bunge ikiwamo posho za wajumbe ambazo ni Sh 300,000 kwa siku kwa mjumbe.
"Fedha zote hizo zilikuwapo katika Bajeti ya Serikali iliyopitishwa Juni mwaka jana, kwa hiyo siyo suala geni. Na zimetumika katika ukarabati wa jengo la ukumbi, vifaa vikiwamo viti 678 ambavyo gharama yake ni dola za Marekani milioni moja," 
“Haya yote mliyoyaona yamefanyika hapa ni mambo ya kawaida ambayo yalikuwa kwenye bajeti la Bunge la Muungano wa Tanzania... si mambo mapya, yalikuwa tu yapo kwenye mchakato, sasa yote yamefanyika kwa wakati mmoja
alifafanua Katibu wa Bunge.
http://www.majira.co.tz/images/upload/Posho%20%20KATUNI%20PG6(70).jpg

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname