Stori: Brighton Masalu
SIKU chache baada ya Bodi ya Filamu
Tanzania (TFB) kuzuia filamu ya mkongwe katika sinema za Kibongo,
Mahsein Awadh Said ‘Dk. Cheni’ ijulikanayo kwa jina la Nimekubali
isiingie sokoni kwa madai kuwa imekiuka maadili ya Kitanzania, msanii
huyo ameibuka na kueleza kinagaubaga, Risasi Jumamosi limenasa sauti
yake.
Akizungumza na mwandishi wetu Jumatano
ya wiki hii maeneo ya Mlimani City jijini Dar, msanii huyo alisema
amesikitishwa na maamuzi ya bodi hiyo huku akidai kuwa lengo la filamu
hiyo ni kukemea tabia za kishoga zinazoendelea kuibuka kwa vijana ikiwa
ni pamoja na kupinga uhalali wa ndoa za jinsia moja
Katika maelezo hayo, DK. Cheni ambaye
huzitendea haki filamu zake kwa kuvaa uhusika halisi, alisema moja ya
kigezo ambacho bodi hiyo imekitumia kuzuia filamu hiyo ni pamoja na
muonekano wa bango la filamu hiyo ambalo linamuonesha msanii huyo akiwa
amevaa vazi la shera huku akiwa amejiremba kwa madai kuwa ni kuchochea
ushoga jambo ambalo msanii huyo amelipinga vibaya.
“Eti ushoga wangu uko kwenye kujiremba
sana, hakika wamenionea sana, lengo letu ni kuonya na kukemea vikali
vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja, huwezi kuelimisha bila
kuonesha madhara yake kwa vitendo kama ilivyo ndani ya filamu hiyo.
“Lakini, ndani ya filamu hiyo, kuna
kipande ambacho kinaonesha kiongozi wa serikali akikemea kitendo hicho,
sasa hapo ushoga wangu uko wapi? Kuvalia shera kwenye kava? Siyo
sahihi,” alisema Dk. Cheni.
Mbali na kava hilo, msanii huyo alidai
haoni kosa lolote katika filamu hiyo hivyo ataendelea kupigania haki
yake na kwamba hayuko tayari kuonewa.
Jitihada za kumpa mkurugenzi wa bodi ya
filamu, Joyce Fissoo ili kuelezea juu ya sekeseke hilo, ziligonga
mwamba hadi gazeti hili linaingia mtamboni lakini imedaiwa kuwa bodi
hiyo itasimamia msimamo wake.
Source:Global Publishers

No comments:
Post a Comment