RATIBA NZIMA YA MAZISHI YA MAREHEMU KANUMBA KESHO
KAMATI YA MAZISHI YA MSANII STEVEN CHARLES KANUMBA
Taarifa kwa vyombo vya
habari
APRILI 9, 2012
Msanii wa filamu,
aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla,
Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012,
atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es
Salaam.
Mazishi ya Kanumba,
yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake
kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi
kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda
wote wa Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu
mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika
tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya
milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli
nzima.
RATIBA
Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa
msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi.
Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi
Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa
pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia
saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na
Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa
Muhimbili kwenda Leaders Club.
Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa
Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi
mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo
itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa
watu mbalimbali.
Saa 6:00 mchana,
ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya
hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders
Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia,
utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.
Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata
utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu
watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili
kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu
na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha
kumuaga mpendwa wetu Kanumba.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda
kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu
aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.
K.N.Y
GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI
No comments:
Post a Comment