30 January 2016

Zali la Al Ahly lamshtua Yondani


 
Yondani amesisitiza wamejipanga kwelikweli lakini akaongeza kwamba wakati mwingine hata sala za mashabiki ni muhimu.
ZALI walilopata Al Ahly mbele ya Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2014 pale jijini Cairo, limewashtua wachezaji wa Yanga ambao wakiongozwa beki kisiki, Kelvin Yondani  na sasa wameingia msituni haswa baada ya kuona kwamba Februari 13 watakwenda ugenini nchini Mauritius kuanza kazi.
Yanga itaanzia michuano ya Afrika ugenini msimu huu kwa kucheza na Cercle de Joachim ambapo mechi ya marudiano itacheza Dar es Salaam Februari 27.
Lakini kwenye mashindano ya msimu huu wamo pia Al Ahly ambapo waliwatoa Yanga kwa jumla ya penati 4-3 ambalo hata mashabiki wa Misri walitafsiri kwamba ni zali lao kwavile Yanga ilipambana kiume kuliko misimu iliyotangulia.
Yondani amesisitiza wamejipanga kwelikweli lakini akaongeza kwamba wakati mwingine hata sala za mashabiki ni muhimu.
 “Sala pia inatakiwa kuhusika, Wanayanga wasali ili ikitokea hali kama hiyo tufanye vizuri, penalti ni bahati nasibu na ni vigumu kusema tutafanya vizuri moja kwa moja, lakini tutapambana,” alisema.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Yanga imepoteza mashindano matatu makubwa kutokana na ugonjwa wa kushindwa kupiga penalti unaowakabili nyota wa timu hiyo, jambo linalozua hofu juu ya uwezekano wa timu hiyo kufanya vizuri katika hatua za mtoano za Klabu Bingwa Afrika ambayo mechi zake zikimalizika kwa sare huamuliwa kwa penalti.
Ilianza hivi. Mwaka 2014 Yanga ilifanya vizuri katika mechi za awali kwa kuifanyia dhahama Komorozine ya Comoro na kuvunja rekodi ya kutokuifunga Al Ahly ya Misri kwa miaka zaidi ya 30 lakini mikwaju ya penalti iliiponza timu hiyo na kuondoshwa katika michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika.
Kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ akiwa katika ubora wa juu kwa wakati huo alipangua mikwaju miwili ya Waarabu hao katika mechi ya marudiano nchini Misri baada ya matokeo ya jumla kuwa bao 1-1, lakini wapigaji wa penalti kwa upande wa Yanga walikumbwa na kigugumizi na kushindwa kutumia fursa hiyo kufunga.
Ugonjwa huo umeonekana kukua siku za hivi karibuni ambapo Yanga imepoteza mataji ya Kagame na Mapinduzi baada ya kuondoshwa katika hatua za robo fainali na nusu fainali kwa mikwaju hiyo ya penalti.
Katika michuano ya Kagame, Yanga iliponzwa na penalti baada ya nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kushindwa kufunga mkwaju wa kwanza wa Yanga katika michuano hiyo dhidi ya Gor Mahia jambo ambalo liliwaponza pia baadaye kwa kuondoshwa na Azam kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya robo fainali.
Licha ya Yanga kujisahihisha na kuifunga Azam kwa penalti katika mechi ya Ngao ya Jamii, bado ilishindwa kutamba kwa mikwaju hiyo katika kombe la Mapinduzi baada ya kuondoshwa na URA katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti pia.
WACHEZAJI

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname