29 January 2016

MKURUGENZI MKUU NIDA ALINUNUA MTAA MZIMA DARSiku mbili baada ya Rais Magufuli kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Bwana Dickson Maimu (pichani kulia) na wakurugenzi waandamizi wa Mamlaka hiyo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka pia kuna tuhuma kuwa katika muda mfupi ambao Bwana Maimu ameiongoza Mamlaka hiyo ameweza kujilimbikizia mali kiasi cha kununua mtaa mzima katika maeneo ya Mikocheni ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba kadhaa za kupangisha.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimethibitishwa na TAKUKURU ni kwamba tayari Taasisi hiyo ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini imeanza kushughulikia suala la NIDA ikiwa ni pamoja na kutaka kupata ukweli na mbinu wanazotumia viongozi wa umma kutajirika katika muda mfupi mara wanapopata madaraka.
“Siyo kosa kwa viongozi kuwa matarajiri lakini inatia shaka unapoona utendaji wa Taasisi unadorora huku utajiri wa viongozi wa Taasisi husika ukikua kwa kasi. Na hili limekuwa jambo lililozoeleka katika sekta ya Umma, TAKUKURU tumejiandaa kupambana na tatizo hili” kimesema chanzo cha kuaminika ndani ya TAKUKURU.
Akizungumzia taarifa hii Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bwana Charles Kitwanga (pichani kushoto) amesema ‘mambo ndani ya NIDA yanazua maswali mengi. Sio utajiri tu wa viongozi wa NIDA ambao unatia shaka bali hata ukweli kuwa katika miaka mitatu NIDA imetumia takribani sh. bilioni 179/= kutoa vitambulisho milioni 2.5 tu tena katika sehemu chache sana za nchi wakati Tume ya Uchaguzi (NEC) iliweza kutoa vitambulisho zaidi ya milioni 20 katika nchi nzima kwa muda wa chini ya miezi mitano !”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname