26 January 2016

HAYA NDO MAMBO 10 YATAKAYO LETA VITA KATI YA CCM NA UKAWA BUNGENI



Spika wa Bunge,Job Ndugai


Dodoma/Dar. Mpambano rasmi wa CCM na Ukawa katika Bunge la Kumi na Moja unaanza kesho huku mambo 10 yakielezwa yataibuliwa na kuchangamsha mjadala unaotarajiwa kuwa wa aina yake katika kipindi cha siku 11 cha bunge hilo.

Katika mambo hayo kumi yanayotajwa kuwa yataibua mjadala mkali bungeni, inaonekana mambo manne yapo dhahiri kutokana na vyama vinavyounda Ukawa kukutana zaidi ya mara tatu kuyajadili.

Mkutano huo wa pili wa Bunge la Kumi na Moja utakuwa wa wiki mbili, lakini uliojaa matukio makubwa kama mabishano ya muundo wa Kamati za Bunge, uchaguzi wa marudio Zanzibar, upinzani kuzuiwa kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi na kuahirishwa kwa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Mambo hayo ni mbali na zile hoja sita, ukiondoa moja ya Zanzibar, zilizoelezwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa katika gazeti hili wiki iliyopita, ikiwa ni matarajio yao kuhusu yatakayojitokeza katika Bunge linaloanza kesho.

Mambo mengine yaliyotajwa na wachambuzi wiki iliyopita ni sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, Hotuba ya Rais John Magufuli, bomoabomoa, Sera ya elimu bure, uchaguzi wa Zanzibar, Katiba mpya na maagizo mbalimbali ya mawaziri.

Kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar ndiyo linaonekana suala kubwa baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Kurudiwa kwa uchaguzi huo kunapingwa na CUF na vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.

Wabunge wa Ukawa walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakati mpinzani wake, Rais Ali Mohamed Shein akiingia kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kusikiliza hotuba ya Rais John Magufuli Novemba 20, mwaka jana.

Zanzibar

Suala la Zanzibar linakolezwa zaidi na kikao kati ya Maalim Seif na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa waliotarajiwa kufanya kikao na wabunge wa Ukawa katika ukumbi wa African Dream jana jioni mjini Dodoma.

Jana kwa nyakati tofauti wabunge wa Ukawa walisita kuzungumzia suala hilo, huku wakishauri watafutwe viongozi wakuu ili kutoa ufafanuzi, hali iliyoashiria kuwa wanasubiri maazimio ya pamoja ya Ukawa ambayo yametajwa kuwa ndiyo utakuwa msimamo wao wa mwisho kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kuwa msimamo wa vyama vinavyounda umoja huo ni kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Alisema kitakachoikumba Zanzibar kwa kulazimisha uchaguzi huo kitamfikisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha mahakamani.

CUF ambayo inapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo, imepanga kufanya vikao vyake vya juu mapema wiki hii kuweka msimamo wake kuhusu tangazo la tarehe ya uchaguzi. Vikao hivyo vitaanza Jumatano.

Muundo Kamati za Bunge

Suala jingine ambalo linaonekana litaibua mjadala katika bunge hilo ni jinsi Ukawa inavyopinga wajumbe wa kamati mbalimbali za bunge walivyoteuliwa na hata kusababisha wasusie uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo.

“Wasemaji wote wamepelekwa kamati ndogo. Serikali inataka kuliendesha Bunge. Hatuhukumu watu lakini unapowaweka katika kamati moja wabunge waliokuwa vinara katika kamati za Bunge lililopita ni ishara ya kutaka kuficha mambo fulani,” alisema Halima Mdee, mbunge wa Kawe kwa tiketi ya Chadema.

Mdee alisema wabunge makini, wenye tabia ya kuibua mijadala na hoja kubwa wamepelekwa katika kamati ambazo hazijadili masuala makubwa ya kitaifa.

Siku tatu zilizopita Bunge lilitangaza wajumbe wa kamati za Bunge, huku likiunda kamati mpya mbili, kubadilishwa majina na nyingine kuunganishwa baada ya Rais Magufuli kupunguza idadi ya wizara kwa kuziunganisha.

Uteuzi huo wa wajumbe wa kamati uliofanywa na Spika wa Bunge, Job Ndugai ulilalamikiwa na wabunge mbalimbali, huku wale wa Ukawa wakisusia uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo, zikiwamo za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), ambazo wenyeviti wake lazima watoke upinzani.

Licha ya kamati zote kupata viongozi wake, kamati ya PAC na Laac ambazo lazima ziongozwe na upinzani, hazijapata wenyeviti baada ya wabunge wa Ukawa kususia uchaguzi.

Moja ya kamati zilizowahi kutikisa nchi ni ya PAC ambayo ilifichua ufisadi mkubwa serikalini kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Akaunti ya Tegeta Escrow.

“Unapowapeleka watu hawa (wabunge wadadisi) katika kamati ambazo zitawafanya wakose hoja kubwa za kuchambua na kudadisi kinachoendelea ndani ya nchi ni kama kulifanya Bunge kuwa kibogoyo,” alisema Mdee.

“Serikali imeingilia kwa kiasi kikubwa kupanga majina ya wajumbe wa kamati. Tunajua lilikuwa ni agizo nani akae wapi na nani awekwe wapi. Hili tutalisema maana hata Spika (Ndugai) hakuweza kufanya lolote, ‘list’ nzima alipelekewa, alichokifanya ni kuitangaza,” alidai Mdee.

Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe aliwashutumu wabunge wa Ukawa na kusisitiza kuwa kamati zote zipo sawa na hakuna kamati iliyo bora zaidi.

“Twendeni kwenye hizi hizi kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania, twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki kuwa Bunge tu. Wabunge tusikubali Bunge Kibogoyo, ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na Malaika,” alisema Zitto.

Upinzani kuzuiwa mikutano

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alisema kitendo cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzuia mikutano ya hadhara ni kinyume na Katiba ya nchi inayompa mwananchi uhuru wa kukusanyika na ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa.

Desemba 25, mwaka jana, Majaliwa alisema wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu hawaruhusiwi kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kuwa wanaweza kuvuruga shughuli za maendeleo.

Alisema wakati wa siasa umekwisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi za maendeleo, hivyo Serikali haitaki tena kuona wanaibuka watu kuvuruga na kwamba mikutano ya shukurani itafanywa na wale tu walioshinda kwenye maeneo yao.

“Lazima tumbane bungeni, kwanza kwa kauli yake kama waziri mkuu, lakini pili kama kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Lazima tumbane atueleze kuhusu suala hili kwa kina ili tujue alikuwa akilenga nini,” alisema Mnyika.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, chama chochote cha siasa kufanya mikutano ni sehemu ya kazi yake, hivyo kukizuia kufanya hivyo ni kukizuia kufanya shughuli zake zilizopo kisheria.

Uchaguzi wa meya Dar

Mdee alisema Ukawa watatumia mjadala wa hotuba ya Rais Magufuli kuhoji uhalali wa kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, uliokuwa umepangwa kufanyika Jumamosi iliyopita.

“Wizara ya Tamisemi ipo chini ya ofisi ya rais na kimsingi kuahirishwa kwa uchaguzi huu ni lazima rais atakuwa anajua kinachoendelea. Hili linafanyika wakati sheria zipo wazi na zinaeleza kila kitu juu ya masuala ya kufuatwa,” alisema Mdee.

Wakati madiwani wa Ukawa wakijipanga kwa uchaguzi huo, Halmashauri ya Jiji ilitoa taarifa ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo bila kueleza sababu za kufanya hivyo, zaidi ya kusema tu utafanyika katika siku itakayotangazwa baadaye.

“Kunapokuwa na dhamira ya kutaka kuchelewesha uchaguzi huu na ukirejea mbinu chafu walizofanya katika uchaguzi wa meya wa halmashauri ya Ilala na Kinondoni, utabaini kuwa kuna mchezo unachezwa,” alisema Mdee.

Alibainisha kuwa uchaguzi huo umekumbwa na ‘figisufigisu’ kwa sababu CCM wanaogopa Ukawa kufumua madudu ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Uda RT).

“Miradi ya Uda na Dart ipo chini ya Jiji na sisi tukiingia ni lazima kuna vitu lazima vijulikane kiini chake na uhalali wa mchakato wake. Naona kuna hofu kuna uchafu uliofanywa Jiji lilipokuwa chini ya CCM unawapa tabu. Wanajua ikipata nafasi itafumua mikataba yote ya Uda,” alisema.

Alisema nyuma ya pazia ya miradi hiyo kuna vigogo wa CCM na watoto wao na ndio sababu ya kufanyika kwa mizengwe. “Ndiyo maana hawatoi sababu za msingi. Ninachokiona hapa ni Rais Magufuli kuogopa aibu ya Serikali yake. Hatuwezi kukwepa kulizungumza jambo hili,”alisema. Hata hivyo, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Simon Group, Robert Kisena mwishoni mwa wiki alisema hakuna kigogo au familia ya kigogo wa serikali au CCM mwenye ubia katika umiliki wa Uda.

Mwenyekiti huyo alisema nje ya familia yake, mtu mwingine mwenye hisa tano ni waziri wa zamani, Profesa Juma Kapuya na akasisitiza kuwa kampuni yake ya Uda RT ndiyo itakayoendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam.

Tayari wabunge wa CCM na Ukawa wapo bungeni na wamekuwa wakifanya vikao mbalimbali vya ndani kwa lengo la kuwekana sawa kabla ya kuanza kwa bunge hilo kesho.

Kauli za wasomi

Mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda alisema jambo ambalo lina uzito wa kujadiliwa bungeni ni lile la Majaliwa kukataza vyama vya siasa kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi baada ya uchaguzi na mengine ni ya kawaida.

“Suala hilo ni muhimu kwa sababu linakandamiza demokrasia hasa kwa vyama vya upinzani,”alisema Mbunda.

Pia, aligusia muundo wa kamati za Bunge kuwa hiyo ni ishara kuwa Serikali imejipanga kutengeneza mazingira ya kutaka sera zake zipite bila vikwazo.

“Hata kwenye mchakato wa naibu spika tuliona…ila kama ni kwa nia njema basi yale yatakayopitishwa na kamati yatakuwa mazuri kinyume na hapo wananchi wataumia,”alisema Mbunda.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dk Charles Kitima alisema kwa kuwa Bunge linaongozwa na sheria, linapokwenda kujadili masuala hayo lazima lizingatie hilo.

“Tunategemea masuala yatakayokwenda kujadiliwa yatazingatia utawala wa sheria,”alisema Dk Kitima.

Alisema Tanzania imekuwa ikifanya maamuzi yake bila kuwagawa wananchi, hivyo hata Bunge katika maamuzi yake kuhusu masuala hayo lazima lizingatie yale ya kuwaunganisha wananchi.

Mbali na hilo, alisema mijadala mingine pia inatakiwa kujikita katika changamoto mbalimbali zilizopo kama ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

“Tunafahamu hapa Tanzania, utaifa kwanza na mengine baadaye. Wakajadili mambo yenye manufaa kwa wananchi waliowapa dhamana ya kuwawakilisha bungeni,” alisema.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alianza kwa kuzungumzia muundo wa kamati za Bunge na kusema kuwa kujadili suala hilo ni kupoteza muda wa kujadili mambo muhimu.

Dk Bana alisema anaamini uchaguzi huo uliofanywa chini ya Spika ulizingatia kanuni, hivyo jambo hilo si la kujadiliwa.




Kuhusa suala za Zanzibar, alisema hilo bado lina ukakasi na utata, lakini kinachotakiwa ni kuendelea kwa mazungumzo baina ya viongozi wa visiwani humo huku uchaguzi ukisubiriwa.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname