19 January 2016

Gazeti la Jamhuri Laituhumu Familia ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Kuhusika na Sakata la Uuzwaji wa UDA Kwa bei ya Kutupwa


Nyaraka za ukaguzi wa kina uliofanywa na kampuni ya Philip& Company imebaini kuwa  Khalfan Kikwete ambaye ni mtoto wa rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete ni sehemu ya wamiliki wa kampuni ya Simon Group iliyonunua UDA kwa bei ya kutupwa.

Taarifa kutoka katika nyaraka hizo za ukaguzi zimebainisha kuwa hesabu za mwaka 2008 za kampuni ya Simon Group zilionesha kuwa Khalifan Kikwete ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo pamoja na Robert Simon Kisena.

Imeelezwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliiuzia kampuni hiyo hisa za UDA bila kufuata utaratibu na sheria huku hesabu zake zikionesha utata mkubwa.

Ukaguzi huo ulionesha kuwa Simon Group haikuwa na uzoefu katika biashara ya usafirishaji wa abiria. Lakini pia hesabu zake za mwaka 2007 zilishangaza baada ya kuonesha kuwa ilipata faida ya shilingi bilioni 1 baada ya kufanya kazi kwa mwezi mmoja tu (Kuanzia Novemba 2007 hadi Desemba 2007).

Hesabu hizo zilichanganya zaidi baada ya kampuni hiyo kuonesha kuwa na hesabu za mwaka mzima wa 2007 wakati imesajiliwa na kuanza biashara mwezi Novemba 2007. Taarifa yake ya hesabu pia haikuonesha kuwepo kwa uchakavu ili hali inamiliki vifaa kama magari na kompyuta.

Katika hatua nyingine, Ukaguzi huo umebaini kuwepo kosa la jinai kwa kampuni hiyo ya Simon Group kukwepa kulipa kodi. Kati ya faida ya shilingi bilioni 1.7, walilipa kodi ya shilingi 225,000 tu, kinyume cha sheria ya kodi inayoitaka kampuni kulipa asilimia 30 ya faida iliyopata, ambayo kwa Simon Group ingekuwa shilingi milioni 510.

Hata hivyo, Robert Simon Kisena aliyetajwa kuwa mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Simon Group alipoulizwa na mwandishi wa Jamhuri, alieleza kuwa hamfahamu mtu anayeitwa Khalfan Kikwete na kwamba kampuni hiyo inamilikiwa na familia yake (familia ya Simon) kwa asilimia 100.

Naye Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam alieleza kuwa hakuhusika na uuzwaji wa UDA na kwamba ulifanywa na viongozi waliomtangulia. Alisema yuko tayari kuhojiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili awaeleze ukweli.

PCCB wakija nitashukuru sana ili niweze kueleza ninachokijua, ila wakija hao wanafiki wengine nitawafukuza maana mimi sipendi unafiki. Nataka wakweli waje tu mimi nipo,” alisema Masaburi.

Udaku Special Blog

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname